Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Tanzania, Ujerumani Kushirikiana Kukuza Miundombinu ya Kidijitali na Ubunifu wa Teknolojia


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholas Merinyo Mkapa, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani katika sekta ya TEHAMA, Anga na Usalama wa Mtandao ni muhimu katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini. 

Bw. Mkapa ameyasema hayo leo tarehe 12 Machi, 2026 alipofanya mazungumzo na Wageni kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania wakiongozw na Bi. Julia Kronberg waliotembelea katika ofisi za wizara zilizopo Mtumba, Jijini Dodoma.

Akizungumza katika Kikao hicho, Bw. Mkapa amesema maeneo ya ushirikiano yaliyopendekezwa yanahusisha kujenga uwezo wa wataalamu wa TEHAMA, kubadilishana maarifa na kuimarisha mifumo ya kidijitali serikalini ili kuendana na mahitaji ya uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi duniani.

Vilevile , Bw. Mkapa alieleza kuwa kupitia ushirikiano huo, Tanzania itanufaika na uzoefu wa Ujerumani katika masuala ya usimamizi wa takwimu za kidijitali na uchumi wa kidijitali, jambo litakalosaidia kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi ya kisera. 

“Serikali inalenga kujenga mifumo madhubuti ya usimamizi wa data pamoja na kuimarisha ulinzi wa taarifa ili kuongeza imani ya wananchi na wafanyabiashara katika huduma za kidijitali,” aliongeza Bw. Mkapa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bi. Julia Kronberg, alisema Ujerumani inaona Tanzania kama mshirika muhimu katika maendeleo ya teknolojia na ubunifu barani Afrika. Pia, Serikali ya Ujerumani iko tayari kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo miundombinu ya kidijitali, usalama wa mtandao, pamoja na kukuza mazingira ya ubunifu na biashara za Teknolojia.

Bi. Kronberg aliongeza kuwa ushirikiano huo utalenga kuimarisha mifumo ya ubunifu na kuunga mkono vijana wabunifu pamoja na kampuni changa za teknolojia (startups) ili ziweze kuendeleza suluhisho za kidijitali zinazokidhi mahitaji ya maendeleo ya Tanzania. 

Alibainisha kuwa Ujerumani ina nia ya kusaidia Tanzania katika kuendeleza miundombinu ya mawasiliano ikiwemo upanuzi wa huduma za intaneti katika maeneo ya vijijini, kuimarisha usalama wa mifumo ya kidijitali pamoja na kutumia teknolojia za kisasa kama satelaiti na data za uchunguzi wa anga kusaidia sekta kama kilimo, mazingira na kukabiliana na majanga.