Habari
TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA VIETNAM KATIKA TEHAMA NA UCHUMI WA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu, Hanoi, Viet Nam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Serikali ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam katika Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa lengo la kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kukuza uchumi wa kidijitali na kuimarisha ustawi wa wananchi wa mataifa hayo mawili.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (MB) wakati wa mazungumzo na Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Vietnam, Mhe. Vu Hai Quan, katika ziara ya Kikazi ambapo alisisitiza utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana kwa karibu na Vietnam katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya teknolojia na ubunifu.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Kairuki alieleza kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vietnam umejengwa kutokana na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Ho Chi Minh, tangu mwaka 1965. Huku akiongeza kuwa, viongozi hao waliamini kuwa uhuru wa taifa na ujamaa ni misingi isiyotenganishwa, na kuhimiza kujitegemea kama nguzo ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Katika mazungumzo hayo, Tanzania ilieleza utayari wake wa kushirikiana na Viet Nam katika maeneo ya maendeleo ya Akili Unde, miji janja, huduma za kompyuta wingu (cloud computing), ubunifu wa kidijitali, maendeleo ya kampuni changa za teknolojia (startups), pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa TEHAMA.
Aidha, Waziri Kairuki aliomba ushirikiano katika sekta zinazotumia teknolojia kwa kiwango kikubwa ikiwemo biashara za kidijitali, biashara mtandao (e-commerce), teknolojia za kilimo (agritech) na nishati jadidifu, ikieleza kuwa ushirikiano huo utafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia.
Vilevile, aliongeza kuwa Tanzania inaendelea kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta ya TEHAMA na kwamba ushirikiano na Viet Nam utasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya uchumi wa kidijitali na kuinua ushindani wa taifa katika mapinduzi ya nne ya viwanda.
Waziri Kairuki alieleza kuwa Tanzania inaendelea kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji barani Afrika na ni mahali salama na penye mazingira rafiki kwa wawekezaji kutoka Vietnam wanaotaka kupanua shughuli zao katika sekta za kimkakati zitakazochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
