Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA, QATAR ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA TEHAMA


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dar es Salaam 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Al Marekhi, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti, 2025, Waziri Silaa amesema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Mkakati wa Miaka 10 wa Uchumi wa Kidijitali, uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 2024 imeweka kipaumbele katika kujenga mazingira wezeshi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Amesisitiza kuwa TEHAMA ni kichocheo muhimu cha maendeleo katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na eneo la ubunifu na kampuni changa ambao imeonesha kuwa sehemu inayoongeza ajira kwa wingi nchini. 

Mazungumzo hayo yameweka msingi wa ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Tanzania na Qatar, huku ikitarajiwa kuwa ushirikiano huo hayo utatoa mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo ya Sekta ya TEHAMA.