Habari
TANZANIA NA SINGAPORE ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA TEKNOLOJIA ZA KIDIJITALI
Na Mwandishi wetu, WMTH- Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Jamhuri ya Singapore uliolenga kuimarisha ushirikiano katika masuala yahusuyo Sekta ya Mawasiliano na TEHAMA nchini.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika tarehe 28 Aprili, 2026 jijini Dodoma, Ujumbe kutoka Jamhuri ya Singapore uliongozwa na Bw. Adrian NG ambaye ni Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Asia, Mashariki ya Kati na Afrika kutoka Wizara ya Biashara na Viwanda.
Bw. Adrian NG alieleza kuwa ziara hiyo ililenga kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ili kuimarisha masuala yahusuyo Sekta ya TEHAMA katika kukuza matumizi ya Teknolojia za kidijitali katika huduma za serikali mtandao, matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali pamoja na utambulisho wa kidijitali ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Vilevile, mazungumzo hayo yalihusisha masuala ya ulinzi na ubadilishanaji wa data, ambapo nchi hizo zilionesha nia ya kushirikiana kuimarisha mifumo salama ya kuhifadhi na kubadilishana taarifa pamoja na kukuza ujasiriamali na start-ups za TEHAMA, ambapo ushirikiano huo utahusisha uwekezaji, mafunzo na ushauri kwa wabunifu wa teknolojia ili waweze kushindana katika soko la kimataifa.
Kwa ujumla, ushirikiano huo unatarajiwa kuharakisha mabadiliko ya kidijitali nchini na kuiwezesha Tanzania kunufaika na uchumi wa kidijitali wa dunia.
