Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA NA PAKISTAN ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA KUHARAKISHA MAGEUZI YA KIDIJITALI


Geneva, Uswisi

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari ili kuharakisha mageuzi ya kidijitali, hususan katika maeneo ya huduma za intaneti ya kasi, Usalama wa Mtandao, Akili Unde (AI), Huduma za Umma za Kidijitali na maendeleo ya Kampuni Changa za ubunifu (startups).

 

Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao kati ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), na Waziri wa Shirikisho wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan, Mhe. Shaza Fatima Khawaja kilichofanyika pembezoni mwa Kongamano la Dunia kuhusu Jamii ya Habari (WSIS) linaloendelea jijini Geneva, Uswisi.

 

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Kairuki aliwasilisha vipaumbele vya Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa ajenda ya mageuzi ya kidijitali, ikiwemo kufikisha huduma za intaneti ya kasi kwa wananchi wote, kupanua huduma za umma zinazotolewa kidijitali, kuimarisha mifumo ya utambulisho wa kidijitali, kuendeleza usalama wa mtandao na mifumo ya kujenga uaminifu katika matumizi ya teknolojia, pamoja na kuimarisha ujuzi wa kidijitali kwa wananchi, hususan vijana, katika matumizi na maendeleo ya akili mnemba.

 

Aidha, Mhe. Kairuki alieleza hatua zinazoendelea za Serikali katika kuanzisha Mfuko wa Kidijitali wa Taifa (National Digital Wallet) na kusisitiza dhamira ya Tanzania kujifunza uzoefu wa Pakistan katika maendeleo ya mifumo ya malipo ya kidijitali na ujenzi wa mifumo jumuishi ya huduma za kidijitali.

 

Akizungumzia juhudi za Serikali za kupanua huduma za mawasiliano nchini, Mhe. Kairuki alipendekeza kuimarishwa kwa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya upanuzi wa intaneti ya kasi vijijini na maeneo ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu kupitia ujenzi wa minara ya mawasiliano, upanuzi wa miundombinu ya nyaya za mawasiliano za fibre optic, pamoja na utekelezaji wa mikakati ya huduma kwa wote ili kuhakikisha makundi yote ya jamii, ikiwemo watu wenye ulemavu, yanapata huduma za mawasiliano.

 

Kwa upande wake, Mhe. Shaza Fatima Khawaja alieleza mafanikio yaliyopatikana nchini Pakistan katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali. Alibainisha kuwa miunganisho ya Fiber-to-the-Home (FTTH) imeongezeka kwa kasi tangu mwanzoni mwa mwaka 2024, huku idadi ya minara ya mawasiliano iliyounganishwa na mtandao wa fibre optic ikiongezeka kutoka asilimia 14 hadi takribani asilimia 20, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufikia asilimia 60 katika kipindi kijacho.

 

Aidha, alisema Pakistan imeanza kutoa huduma za teknolojia ya 5G katika miji 22 kupitia uwekezaji mkubwa katika mifumo ya nyaya za mawasiliano chini ya bahari (submarine cable systems) na njia mbadala za mawasiliano ya ardhini, hatua zilizoongeza uimara na uhakika wa huduma za mawasiliano nchini humo.

 

Katika eneo la utawala wa kidijitali, Pakistan ilishirikisha uzoefu wake katika kuanzisha mifumo ya utambulisho wa kidijitali, jukwaa la kitaifa la kubadilishana taarifa, programu jumuishi za huduma kwa wananchi pamoja na majukwaa ya kidijitali yanayohudumia sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo na huduma za kifedha.

 

Mawaziri hao pia walijadili masuala ya usalama wa mtandao na kukubaliana kuwa eneo hilo ni nguzo muhimu katika kulinda mifumo ya kidijitali na kuimarisha usalama wa taifa. Katika hilo, Pakistan ilipendekeza kuanzishwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Timu za Taifa za Kukabiliana na Dharura za Usalama wa Mtandao (CERTs) za nchi hizo mbili kupitia mafunzo ya pamoja, mazoezi ya kukabiliana na matukio ya kimtandao pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu ulinzi wa taarifa na mifumo ya udhibiti wa kidijitali.

 

Katika kukuza uchumi unaotokana na ubunifu, Tanzania na Pakistan pia zilikubaliana kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya kampuni changa za ubunifu na ujasiriamali wa kidijitali. Tanzania ilieleza kuwa ipo katika hatua za mwisho za kuandaa Sera ya Taifa ya Kampuni Changa za Ubunifu na kwamba takribani asilimia 60 ya kampuni hizo zinafanya shughuli zake katika sekta ya TEHAMA. Kutokana na hali hiyo, Tanzania imeonesha nia ya kujifunza uzoefu wa Pakistan katika kuandaa sera na mifumo ya kujenga mazingira wezeshi kwa ubunifu na biashara za teknolojia.

 

Mwishoni mwa kikao hicho, Mawaziri hao walisisitiza dhamira ya Serikali za nchi zao kuendeleza ushirikiano wa karibu katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari na kukubaliana kuanza mchakato wa kuunda Kikundi Kazi cha Pamoja cha Kiufundi (Joint Technical Working Group) kitakachosimamia utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwa lengo la kuyageuza kuwa miradi na programu zenye manufaa kwa wananchi wa nchi zote mbili.