Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA NA OMAN KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA MAWASILIANO, HABARI NA TEKNOLOJIA


               

  • Waziri wa Habari wa Oman akubali kutumia vyombo vya  Habari vya Oman kuitangaza  Tanzania      
  • Tanzania kushirikiana na Oman katika Sekta ya usafirishaji na Mawasiliano

Tanzania na Oman zaweka mikakati ya ushirikiano katika sekta ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ambapo nchi hizi mbili zinaweza kutumia vyombo vyake vya habari kuhabarisha umma katika masuala mbalimbali ya kijamii, kutangaza tamaduni na kubadilishana ujuzi wa teknolojia.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye wakati alipokutana na Waziri wa Habari wa Oman Mhe. Dkt. Abdullah bin Nasser bin Khalifa Al-Harassi tarehe 23 Novemba, 2022, nchini Oman.

Katika mazungumzo yao Waziri Mhe. Nape ameeleza kuwa, kutokana na mahusiano ya kihistoria ya muda mrefu kati ya Tanzania na Oman, nchi hizi zinapaswa kuhabarishwa ipasavyo juu ya undugu wa damu kati ya watu wa Oman na watanzania ili kuendelea kutunza uhusiano huo na kukubaliana kuwa Oman kupitia vyombo vyake vya habari itaitangaza Tanzania katika mataifa mengine ili kuvutia biashara, uwekezaji na utalii. 

Aidha, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye ametembelea chumba maalum kinachotumika katika shughuli za uandaaji wa habari za magazeti, Radio na Televisheni kwa lengo la kufahamu uandaaji wa vipindi nchini humo.

Katika hatua nyingine, Waziri Nape amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uchukuzi, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Oman Mhe. Mhandisi Saeed Bin Hamoud bin Saeed Al Maawali huku Waziri wa Oman akiahidi kuendelea kuipa ushirikiano Tanzania katika Sekta ya Usafirishaji na Mawasiliano hususani katika masuala ya usalama mitandaoni (Cyber Security).

Vilevile Mhe. Nape alipata nafasi ya kutembelea maghala yanayomilikiwa na kampuni ya ASYAD EXPRESS na yanayotumika kutunzia bidhaa kwa ajili ya kusambaza na kuuza kwa wananchi kupitia biashara mtandao nchini Oman.

Sambamba na hilo, Mawaziri hao wawili wa Serikali ya Oman wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha Habari; Mawasiliano na Teknolojia ya Usafirishaji kwa manufaa ya nchi hizi mbili.