Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA NA KAZAKHSTAN ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI KATIKA KUENDELEZA MAGEUZI YA KIDIJITALI


Na Mwandishi wetu

Geneva, Uswisi

 

Tanzania na Kazakhstan zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika mageuzi ya kidijitali, hatua inayofungua fursa za ushirikiano mpana zaidi katika maeneo ya Akili Unde (AI), huduma za umma kidijitali, upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano ya intaneti ya kasi (broadband), usalama wa mtandao, ubunifu, maendeleo ya kampuni changa za teknolojia (startups), pamoja na ujuzi wa kidijitali.

 

Makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa mkutano wa ngazi ya juu kati ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Angellah Mbelwa Kairuki (Mb) na Naibu Waziri Mkuu wa Kazakhstan Mhe. Zhaslam Madiyev, uliofanyika mjini Geneva, Uswisi.

 

Katika mazungumzo hayo, Kazakhstan iliwasilisha mafanikio yake katika mageuzi ya kidijitali, ikieleza kuwa takribani asilimia 92 ya huduma zote za Serikali zinapatikana kwa njia ya mtandao.

 

Aidha, Mhe. Madiyev alieleza mpango wa nchi hiyo wa kupanua huduma za mtandao wa 5G kufikia kati ya asilimia 60 na 75 ya miji yake mikubwa ifikapo mwisho wa mwaka ujao, ikiwa ni sehemu ya safari yake kuelekea uchumi wa kidijitali unaotegemea kikamilifu teknolojia za kisasa.

Kazakhstan pia iliwasilisha dira yake ya kuwa kitovu cha kimataifa cha Akili Unde kupitia kuanzishwa kwa Kituo cha Kimataifa cha AI pamoja na ujenzi wa mfumo wa vituo vya kuhifadhi na kuchakata taarifa za AI (AI Data Centres) wenye uwezo wa gigawati moja.

 

Mpango huo unajumuisha mradi wa awali wenye uwezo wa megawati 250 wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 10, utakaotumia vitengo 100,000 vya uchakataji wa picha (Graphics Processing Units – GPUs), ambapo utekelezaji wake utafanyika kwa awamu mbili kuanzia mwaka ujao hadi mwaka 2028.

 

Kwa upande wake, Mhe. Kairuki alipongeza mafanikio hayo na kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kuharakisha utekelezaji wa ajenda yake ya mageuzi ya kidijitali. Alieleza vipaumbele vya Tanzania kuwa ni kupanua upatikanaji wa mawasiliano kwa wote kupitia huduma za broadbandi, kuboresha huduma za serikali kidijitali (e-Government), kuimarisha usalama wa mtandao, kujenga ujuzi wa kidijitali kwa wanawake, vijana na makundi maalum, pamoja na kujenga mfumo imara wa ubunifu na ukuaji wa kampuni changa za teknolojia.

 

Mhe. Kairuki pia aliwasilisha Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (National e-Procurement System – NEST), akieleza kuwa mfumo huo tayari umeunganisha mifumo 21 ya Serikali na umeongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa michakato ya ununuzi wa umma.

 

Alipendekeza ushirikiano katika matumizi ya Akili Unde kuboresha mfumo huo kupitia utambuzi wa udanganyifu, kuongeza uwazi, kurahisisha tathmini ya zabuni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa sera ya Serikali inayotenga angalau asilimia 30 ya fursa za zabuni kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

 

Kwa upande wake, Kazakhstan imeeleza utayari wake wa kushirikiana na Tanzania huku pande zote mbili zikikubaliana kuanzisha vikundi vya pamoja vya wataalamu, kuwezesha kubadilishana uzoefu kati ya taasisi husika, kuandaa ziara za mafunzo, pamoja na kushiriki kwa pamoja katika majukwaa ya kimataifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Akili Unde.