Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA NA BRAZIL ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA MAGEUZI YA KIDIJITALI


Na Mwandishi wetu Geneva, Uswisi.

 

Tanzania na Brazil zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuharakisha mageuzi ya kidijitali kupitia maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano, usalama wa mtandao, matumizi ya akili unde (AI), ubunifu na uwekezaji katika teknolojia.

 

Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao kati ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki(Mb.) na Balozi wa Teknolojia wa Brazil, Mhe. Eugenio V. Garcia, kilichofanyika pembezoni mwa Kongamano la Kimataifa kuhusu Jamii ya Habari (WSIS) mjini Geneva, Uswisi.

 

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilijadili fursa za kuimarisha ushirikiano katika mageuzi ya kidijitali, huduma za serikali kidijitali, usalama wa mtandao, akili unde na maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

 

Waziri Kairuki alipendekeza kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) itakayoweka msingi wa ushirikiano huo, huku akiialika Brazil kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji wa vituo vya kuhifadhi taarifa (Data Centres) na maendeleo ya kampuni changa za teknolojia.

 

Kwa upande wake, Balozi wa Teknolojia wa Brazil, Garcia, alieleza utayari wa nchi yake kushirikiana na Tanzania kwa kushirikisha uzoefu katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Akili Unde, jukwaa la huduma za serikali kidijitali la Gov.br, mfumo wa malipo wa papo kwa papo wa PIX, pamoja na miradi ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini.

 

Pande hizo mbili pia zilikubaliana kuimarisha ushirikiano katika usalama wa mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi, kubadilishana wataalamu na uzoefu, pamoja na kuendelea kushirikiana ndani ya Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) ili kuendeleza ajenda ya mageuzi ya kidijitali na maendeleo endelevu.