Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Tanzania, Burundi Zasaini Makubaliano ya Kibiashara katika Mkongo wa Mawasiliano


 

 

Na Mwandishi Wetu-WHMTH

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), amelielekeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora za mawasiliano.

Ametoa kauli hiyo, februari 23, 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Burundi Backbone System (BBS) uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.

Mkataba huo mpya wa kibiashara kati ya TTCL na BBS wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 3.3, sawa na shilingi za kitanzania bilioni 8.3 ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiteknolojia kati ya Tanzania na Burundi, na kufungua njia ya ushirikiano mpana zaidi katika sekta ya mawasiliano.

Mhe. Nape amebainisha kuwa matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano nchini yamepelekea Serikali ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo.

Waziri Nape amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake thabiti ya kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati kama njia ya kufanikisha maendeleo.

Mhe. Nape amewakaribisha Burundi kutumia Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) kilichopo Tanzania ambacho ni miongoni mwa vituo bora barani Afrika, kinachotumia teknolojia za kisasa, na kina usalama wa kutosha.

Mkataba huo wa ushirikiano umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga, na Mkurugenzi Mkuu wa BBS, Bw. Jeremie Diomede Hageringwe.