Habari
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Poland Zaongeza Ushirikiano katika Mageuzi ya Kidijitali na Akili Unde (AI)
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amefanya mazungumzo ya pande mbili na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Masuala ya Kidijitali wa Jamhuri ya Poland, Mhe. Krzysztof Gawkowski, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika mageuzi ya kidijitali, usalama wa mtandao, Akili Unde (AI), na huduma za umma za kidijitali.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Angellah Kairuki aliwasilisha vipaumbele vya Tanzania katika mageuzi ya kidijitali, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wote, utambulisho wa kidijitali, usalama wa mtandao, maendeleo ya ujuzi wa kidijitali, matumizi ya Akili Unde (AI), ujumuishaji wa kidijitali, pamoja na upanuzi wa huduma za umma zinazotolewa kwa njia za kidijitali. Aidha, alipendekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Poland katika maeneo ya usalama wa mtandao, serikali ya kidijitali, utafiti na usimamizi wa Akili Unde (AI), upanuzi wa miundombinu ya intaneti ya kasi (broadband), pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu. Pia alieleza nia ya Tanzania kujifunza kutokana na uzoefu wa Poland katika matumizi ya pochi za kidijitali (digital wallets), mifumo ya kushirikiana kwa majukwaa ya kidijitali (interoperability), na mifumo ya malipo ya kidijitali.
Kwa upande wake, Mhe. Gawkowski alipokea mapendekezo hayo kwa mikono miwili na kueleza kuwa vipaumbele vya Tanzania vinaendana kwa karibu na mkakati wa Poland wa maendeleo ya kidijitali. Alithibitisha utayari wa Poland kushirikiana na Tanzania kwa kubadilishana uzoefu katika serikali ya kidijitali, usalama wa mtandao, ulinzi wa miundombinu muhimu, suluhisho za malipo ya kidijitali na Akili Unde (AI). Aidha, alipendekeza kuandaliwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kuhusu ushirikiano wa kidijitali na kuwaalika wataalamu wa Tanzania kuanza majadiliano ya kiufundi na wenzao kutoka Poland.
Akihitimisha mazungumzo hayo, Mhe. Gawkowski alimwalika Mhe. Angellah Kairuki kufanya ziara rasmi ya kikazi nchini Poland ili kuendeleza ushirikiano wa pande mbili na kuchunguza uwezekano wa kusaini Hati ya Makubaliano iliyopendekezwa.
Mazungumzo hayo yamedhihirisha dhamira ya pamoja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Poland ya kujenga ushirikiano wa muda mrefu unaochochea mageuzi ya kidijitali yaliyo salama, jumuishi na yenye ubunifu kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
