Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA BARAZA LA KIMATAIFA LA USHAURI KUHUSU UIMARA WA NYAYA ZA MAWASILIANO ZINAZOPITA CHINI YA BAHARI NCHINI USWISI


Geneva, Uswisi

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ameshiriki katika mkutano wa mwisho wa Baraza la Kimataifa la Ushauri kuhusu Uimara wa Nyaya za Mawasiliano Zinazopita Chini ya Bahari (International Advisory Body on Submarine Cable Resilience), uliofanyika Geneva, Uswisi, kandokando ya Kongamano la ITU WSIS+20 Forum 2026 pamoja na Mkutano wa AI for Good Global Summit 2026.

Baraza hilo, lililoanzishwa mwaka 2024 na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) kwa kushirikiana na Kamati ya Kimataifa ya Ulinzi wa Nyaya za Mawasiliano (International Cable Protection Committee – ICPC), linawakutanisha mawaziri, wasimamizi wa sekta, viongozi wa sekta binafsi na wataalamu wa kiufundi kutoka duniani kote kwa lengo la kuimarisha uimara wa nyaya za mawasiliano zinazopita chini ya bahari. Nyaya hizo hubeba zaidi ya asilimia 99 ya data zote zinazopita duniani na ndizo mhimili mkuu wa uchumi wa kidijitali duniani, zikisaidia mawasiliano, huduma za kifedha, biashara, huduma za Serikali, afya na elimu.

Katika mkutano huo wa kuhitimisha shughuli za Baraza, wajumbe walipitisha ripoti ya mwisho ya Baraza hilo, ikiwa ni hitimisho la programu ya kazi ya miaka miwili iliyotekelezwa kupitia mikutano ya kimataifa iliyofanyika Abuja, Nigeria (2025) na Porto, Ureno (2026). Ripoti hiyo inaweka mapendekezo ya vitendo ya kulinda miundombinu hii muhimu na kutoa mwongozo wa pamoja wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na sera za kitaifa.

Mapendekezo hayo yamegawanywa katika maeneo matatu ya kazi. Kundi la kwanza linahusu kuharakisha uwekaji na ukarabati wa nyaya za mawasiliano, ikiwemo kurahisisha utoaji wa vibali na kuhakikisha uwezo wa kutosha wa ukarabati. Kundi la pili linajikita katika kutambua, kufuatilia na kupunguza vihatarishi vinavyozikumba nyaya hizo, ambapo vingi husababishwa na shughuli za uvuvi, kutia nanga kwa meli na majanga ya asili. Kundi la tatu linahusu kuimarisha muunganiko wa mawasiliano na kuongeza njia mbadala za mawasiliano ya kimataifa ili kuhakikisha hakuna nchi au eneo linalobaki katika hatari kutokana na kutegemea mfumo mmoja wa nyaya za mawasiliano.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki alisisitiza umuhimu wa kimkakati wa kuimarisha uimara wa nyaya za mawasiliano zinazopita chini ya bahari katika kufanikisha ajenda ya Tanzania ya mageuzi ya kidijitali na maendeleo ya Bara la Afrika kwa ujumla. Alieleza kuwa mawasiliano ya uhakika kupitia nyaya hizo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania, utoaji wa huduma za umma na ustawi wa wananchi. Aidha, alithibitisha dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kulinda miundombinu hiyo muhimu, kuongeza njia mbadala za mawasiliano na kujenga uwezo wa kitaifa katika ulinzi na ukarabati wa nyaya hizo.

Mhe. Kairuki pia aliipongeza ITU na ICPC kwa uongozi wao katika kuratibu kazi za Baraza hilo na kuikaribisha ripoti hiyo kwa kuzingatia umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, kuongeza njia mbadala za mawasiliano na kuzipa kipaumbele nchi zinazoendelea, hususan mataifa ya visiwa vidogo na nchi zenye maendeleo duni ambazo zinaendelea kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na changamoto za kukatika kwa mawasiliano.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kikanda na kimataifa za kuimarisha uimara wa nyaya za mawasiliano zinazopita chini ya bahari, kwa lengo la kujenga mustakabali wa kidijitali ulio salama, jumuishi na wenye muunganiko imara kwa manufaa ya wananchi wake.