Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YABAINISHA MAFANIKIO YA AI NA UBUNIFU WA KIDIJITALI KATIKA MKUTANO WA WSIS+20


 

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Geneva, Uswisi 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Jerry William Silaa, amebainisha mafanikio makubwa ya Tanzania katika Akili Unde (AI) na mabadiliko ya kidijitali wakati wa mjadala wa ngazi ya juu katika Mkutano wa WSIS+20 unaofanyika Geneva.

Akizungumza katika moja ya mjadala ulioongozwa na mada ya “AI na Dunia Pepe: Kujenga Miji na Serikali za Kesho,” Mhe. Silaa alisisitiza nafasi ya kimkakati ya AI katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania. Alielezea kuhusu Mkakati wa Taifa wa Miaka 10 wa Uchumi wa Kidijitali (2024-2034) uliozinduliwa Julai 2024, unaolenga kukuza maarifa ya kidijitali, uvumbuzi, na utoaji bora wa huduma kwa wananchi kupitia teknolojia ya AI.

“Tanzania inaitumia teknolojia hii kuboresha utoaji wa huduma, kuhimiza ubunifu, na kuwawezesha vijana wetu.”

Waziri Silaa pia alieleza hatua zilizopigwa katika usalama wa mtandao na ulinzi wa taarifa binafsi, akitaja Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 na kuanzishwa kwa Tume ya Taifa ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi mwaka 2023, zenye lengo la kulinda faragha ya raia na kujenga uaminifu katika mazingira ya kidijitali.

Katika hatua ya kukuza ubunifu kwa vijana, Mhe. Silaa aliwaeleza washiriki wa mjadala huo kuwa Tanzania inaendelea na ujenzi wa vituo nane vya ubunifu (innovation hubs) katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo Zanzibar. Vituo hivyo vitatoa nyenzo, mafunzo, na mazingira bora kwa vijana na wajasiriamali kuunda suluhisho za kiteknolojia zenye tija.

Aliongeza kuwa, Tanzania inashirikiana na UNESCO, UNICEF, na Benki ya Dunia kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa AI, ambao utahakikisha matumizi jumuishi na salama ya teknolojia hii, sambamba na viwango vya kimataifa.

“Kwa kushirikiana, tunaweza kujenga mustakabali wa AI wenye manufaa kwa wote,” alihitimisha Mhe. Silaa, huku akisisitiza dhamira ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo ya kiteknolojia.

Mhe. Silaa yuko Geneva ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa Mkutano wa WSIS+20, tarehe 7 Julai ambao utamalizika tarehe 11 Julai 2025. Mkutano huu unawakutanisha viongozi wa kimataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na wataalam wa sera za kidijitali kujadili mchango wa teknolojia katika maendeleo jumuishi na endelevu.