Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TAKRIBANI NCHI 30 ZA UMOJA WA PAPU ZAKUTANA ARUSHA KUSHIRIKI MKUTANO WA 41 WA BARAZA LA UTAWALA


Na Faraja Mpina, WHMTH, Arusha

Nchi za Afrika takribani 30 kati ya 45 ambazo ni wanachama wa umoja wa Posta Afrika, zimekutana jijini Arusha Tanzania kushiriki Mkutano wa 41 wa Baraza la Utawala la Umoja huo.

Mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili jijini Arusha umehitimishwa leo Agosti 30, 2023 na kufungwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed.

Akifunga rasmi Mkutano huo, Dkt. Mohammed amesema kidunia sekta ya posta imekuwa na mabadiliko makubwa kutokana na kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

 Ameongeza kuwa kutokana na kukua kwa TEHAMA bara la Afrika linaweza kutengeneza kesho ambayo mipaka ya nchi zetu sio kikomo cha kununua au kuuza bidhaa katika bara la Afrika kupitia teknolojia ya kidijitali, biashara mtandao na huduma za posta.

“Kinachohitajika ni kuwajengea uwezo wataalamu wetu, kutoa elimu kwa umma na ujenzi wa miundombinu ya kidijitali ili kuunganisha maeneo yote ya mijini na vijijini katika katika nchi zetu, lakini pia kushughulikia usalama wa huduma mtandao kwa lengo la kuboresha biashara mtandao na huduma za posta”, amesisitiza Dkt. Mohammed.

Mkutano huo uliofanyika Arusha Tanzania, ambapo ndipo lilipo jengo la ofisi za Makao Makuu ya Umoja huo linalotarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo Septemba 2, 2023.

Nchi zilizohudhuria Mkutano huo ni pamoja na nchi za Angola, Algeria, Benin, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Congo DRC, Cote D’Ivoire, Egypt, Ethiopia, Ghana, Kenya, Liberia, Madagascar, Malawi, Mali, Morocco, Mozambique, Namibia, Nigeria, Senegal, South Afrika, Uganda, Zimbabwe, Eswatini, Tunisia, Cameroon na Tanzania.