Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TABORA MKAWE VINARA UTEKELEZAJI WA ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI - MHANDISI KUNDO


TABORA

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amewataka Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Tabora kuwa wa kwanza katika utekelezaji wa anwani za Makazi na Postikodi na pia iweze kurahisisha zoezi la Sensa ya watu na Makazi 2022.

 Mheshimiwa Kundo ametoa kauli hiyo leo tarehe leo Jumatatu, Februari 22, 2022 katika kikao kazi cha kuwajengea uwezo Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Tabora kuhusu utekelezaji wa Mfumo wa anwani za Makazi na Postikodi katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora.

 Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi Nchini.

“Msingi wa kutekeleza Mfumo huu, kwanza ni ahadi tuliyoitoa kwa Watanzania kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) kwamba ifikapo 2025 wanachi wote watakuwa na Anwani za Makazi, pili ni matakwa ya Umoja wa Kimataifa ambapo Nchi yetu ni mwanachama wa umoja huo (UPU na PAPU), na tatu ni maelekezo ya Sera yetu ya Posta ya mwaka 2003.”

 “Tarehe 8 Februari, 2022 Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maelekezo kwamba utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ufanyike kwa nia ya operesheni kwa kusimamiwa na Wakuu wa Mikoa na kwamba ukamilike ifikapo Mei 2022. Aidha kwa upande wa Zanzibar, tarehe 20 Februari, 2022 Mhe Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa ,aelekezokwa Wakuu wa Mikoa yote Zanzibar akisisitiza utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais wa Nchi yetu. Hit inaonyesha namna Serikali yetu kupitia viongozi Wakuu wa Nchi wanavyotamani kuona Mfumo huu unakamilika haraka iwezekananvyo.”- amesema Mhandisi Kundo.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda, amesema kuwa Uongozi wa Mkoa wa Tabora ulishafanya kikao cha kwanza na kutoa elimu kwa Wananchi na hivyo utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unaendelea vizuri kwa Mkoa huo na ifikapo mwishoni mwa mwezi April watakuwa wamekamilisha zoezi hilo na kuwa tayari kwa zoezi jingine la Sensa itakayofanyika mwezi Agosti, 2022.

 Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, amesema Chama cha Mapinduzi imepokea na kuunga Mkono jambo hilo la Anwani za Makazi na Postikodi kwani linatokana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya (2020-2025).

 Mfumo wa Anwani za Makazi  ulianza utekelezaji wake mnamo mwaka 2010 chini ya aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.