Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TAASISI 661 KUUNGANISHWA NA MTANDAO WA SERIKALI


Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali imesaini mikataba miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 43.3 ya usimikaji wa vifaa vitakavyowezesha taasisi 661 za umma kuunganishwa na mtandao wa Serikali (GovNET).

Akizungumza katika hafla ya utiaji Saini mikataba hiyo leo Novemba 6 jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema lengo ni kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa njia ya kidijitali kwa kuwa mtandao huo wa Serikali umeunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Mikataba hiyo imesainiwa na Katibu Mkuu kwa upande wa Wizara na Bw. Abdulrazak Seif, Mkuu wa Idara ya Miundombinu ya TEHAMA wa M/S Softnet Technolojies Ltd wenye thamani ya shilingi na 19.4

Mkataba wa pili uliosainiwa ni baina ya Katibu Mkuu na Bw. Saidi Buhero, Mtendaji Mkuu wa m/s Emerging Communications ltd wenye thamani ya shilingi bilioni 17.2

Sambamba na hilo, Katibu Mkuu huyo pia amezindua Kikundi Kazi cha Mapinduzi ya Kidijitali cha baraza la Taifa la Biashara kilichoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi chenye jumla ya wajumbe 16 ambapo wajumbe 8 wanatoka taasisi za umma na 8 wanatoka sekta binafsi.

Katibu Mkuu Abdulla ambaye ndio mwenyekiti wa Kikundi kazi hicho amesema kazi rasmi imeanza leo ambapo watajadili na kushauriana namna bora ya nchi kunufaika na matumizi ya TEHAMA na kuweza kukuza uchumi wa kidijitali.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi inaendelea kujenga na kuimarisha miundombinu ya kidijitali ili kama nchi iweze kufikia mapinduzi ya nne ya viwanda yanayoongozwa na TEHAMA.

“Misingi mikuu ya miundombinu hii ya kidijitali ni kuhakikisha tunakuwa na mifumo bora ya utambuzi wa watu (Digital Identity), ujenzi wa mfumo wa pamoja wa malipo (Digital Payment), na kuweka miundombinu rafiki na yenye usalama katika kubadilishana taarifa”, amesema Katibu Mkuu Abdulla.

Ameyataja maeneo mengine kuwa ni kuwepo kwa majukwaa/mifumo ya Kubadilishana taarifa (Data Exchange Platform), Usalama Mtandao (Cyber Security), Mazingira Wezeshi ya sera, sheria, kanuni na miongozo (Enabling Environment) na eneo la Utafiti na Ubunifu (Research and Innovation).

Amesema kuwa Kikundi Kazi cha Mapinduzi ya Kidijitali cha baraza la Taifa la Biashara kinaenda kujadili maeneo hayo saba kama vipaumbele vya utekelezaji na kuibua mengine ambayo kwa pamoja yakifanyiwa kazi kama Taifa na kuhakikisha mapinduzi ya kidijitali yanakuwa si ndoto.