Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TAARIFA BINAFSI INA JUKUMU LA KULINDA HESHIMA NA HAKI ZA WATU – WAZIRI NAPE


Na Chedaiwe Msuya na Mussa Richard, WHMTH


 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Mosses Nnauye (Mb)  amewataka watumishi wa Tume Ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini (PDPC) kufanya kazi kwa ufanisi na kulinda imani Ya Tume hiyo na kuwaasa kutekeleza Sheria ya Tume bila kuwakera Wateja wao.

Waziri Nape amesema hayo Leo wakati akizindua Bodi ya Tume Ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini (PDPC)) katika Ukumbi wa Mikutano wa TCRA jijini Dodoma.

Katika hatua nyingine Waziri Nape ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan na Watanzania kiujumla wanaimani na Tume hiyo pamoja na Viongozi wake  walioteuliwa Balozi Adadi Mohammed Rajabu kuwa mwenyekiti na Bi. Fatma Mohammed Ali kuwa kaimu  huku akiwataka Viongozi hao kutengeneza Mpango mkakati ili Tume hiyo itoe Huduma za Viwango vya Juu na  huduma hizo zitolewe katika Mfumo wa Kidigitali.

"Mnafahamu kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria Na.11 ya mwaka 2022 ambayo ilianza kutekelezwa tarehe 01 Mei, 2023 hivyo msingi wa majukumu ya Bodi ni kuhakikisha Sheria na kanuni zinatekelezwa kwa ukamilifu lakini bila kuwa kikwazo kwa wateja wa Tume". Amesema

Pia Waziri Nape amewataka Viongozi wa Tume hiyo kutekeleza majukumu yao kwani Tume hiyo ni Tume nyeti katika ukuaji wa Sayansi na Teknolojia  akiongeza kuwa  jambo hilo litafanya watu kutoka mataifa mbalimbali Duniani wakimbilie nchini kwani Tanzania ni nchi Salama.

“Kujitanganza na kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo na majukumu ya Tume kwani kwa sasa bado watu hawafahamu uwepo wa Tume hii hivyo mjipange vyema kusimamia suala hili na kuandaa makongamano ya kikanda na kimataifa ili kuwezesha upatikanaji wa fursa mbalimbali pamoja na wawekezaji “ amesema Waziri Nape

Aidha, Mhe Waziri amesema kuwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ina jukumu kubwa la kulinda heshima na haki za watu kwa kuhakikisha taarifa zao binafsi zinatumika kwa njia inayo zingatia haki, heshima,na utu wa mtu.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Bw.  Emmanuel Mkilia amesema kuwa Malengo ya Tume hiyo yamefikia asilimia 90 katika siku 100 toka Tume hiyo ianze kazi.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi huyo amesema kuwa Malengo ya Tume  hiyo ni Kutengeneza Utambulisho wa Tume kwa kutengeneza machapisho ya Wizara na kujenga jengo la Tume pia akaiomba Serikali kuongeza Wafanyakazi katika Tume kwani mpaka sasa Tume inawafanyakazi 16 pekee.

Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed KHamis Abdulah amewapongeza watumishi wa Tume kwa kusema kuwa wamefanya juhudi kubwa mpaka kufikia kuzinduliwa kwa Tume hiyo haikua rahisi kukamilika katika kipindi cha siku 100 na wahakikishe  watekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya kikanda na kimataifa. 

 Tume hiyo iliundwa mnamo tarehe 1 mwezi wa 5 mwaka 2023 ikiwa na jumla ya Watumishi 12 pekee.