Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SHIRIKA LA POSTA, KAMPUNI YA NDEGE ZA TANZANIA ZASAINI MKATABA WA KIBIASHARA


Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Macrice Mbodo pamoja na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Mhandisi Ladislaus Matindi wakibadilishana hati za makubaliano ya kibiashara kati ya ATCL na TPC nchini mara baada ya kusaini hati hizo katika Makao Makuu ya Shirika la Posta, jijini Dar es Salaam

Prisca Ulomi, WHMTH, DAR ES SALAAM

Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) zimesaini mkataba wa kibiashara leo wa kuziwezesha taasisi hizo za umma kusogeza huduma zake karibu kwa wananchi

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameshuhudia hafla hiyo ya utiaji saini mkataba baina ya taasisi hizo mbili ya TPC na ATCL na kuzindua rasmi ushirikiano huo wa kibiashara ambapo TPC kama wakala wa ATCL imemkatia tiketi ya ndege ya ATCL Waziri Nape papo hapo baada ya uzinduzi huo

“Niwapongeze kwa ubunifu mkubwa mliofanya, na hii imechagiza maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikisha huduma kwa wananchi na muwahamishe wananchi kutumia huduma hizo”, amesema Waziri Nape

Waziri Nape ameongeza kuwa, “ATCL mna mashirika ya ndege mnayofanya nayo kazi, na TPC nao wana mashirika yao huko duniani, hivyo ATCL na TPC wote mtanufaika ni vizuri mkashirikiana na sekta binafsi, acheni kujifungia, tokeni nje, mnachokipata mtagawana na kuongeza tija ya mashirika yenu “.

“ATCL na TPC mkawajibike ipasavyo ili huduma zote za mashirika haya ziwe nzuri zaidi na ubora wa huduma uzingatiwe, hivyo msifumbiane macho, mwambizane ukweli kwa kuwa unapomkamua mtu jipu atapiga kelele ila kesho atapona; ubora wa huduma zenu utavutia sana wateja,” amesisitiza Waziri Nape

Akizungumza wakati anamkaribisha Waziri Nape, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa ajenda kuu ya Wizara hiyo ni kuipeleka Tanzania Kidijitali na mashirikiano baina ya TPC na ACTL ni moja ya njia ya kuifikisha nchi Kidijitali huku akiugusia mfumo wa anwani za makazi kama njia nyingine ya kuipeleka Tanzania Kidijitali

“TPC inategemea usafiri wa haraka, salama na unaoaminika na ATCL inahitaji kufikia wateja wake, hivyo ushirikiano huu ni muhimu,” amesema Abdulla

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Brigedia Mstaafu Yohana Mabongo amesema kuwa bodi itahakikisha ndoa baina ya ATCL na TPC inashamiri ili nchi yetu itoboe katika ya uchumi kwa kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kibiashara uliosainiwa leo hii unaenda kuhudumia wananchi ipasavyo

Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo amesema kuwa TPC imeona fursa ya kutumia ATCL kuwa wakala na kufanya makubaliano ya kibiashara ikiwemo wakala wa kukata tiketi za ndege na usafirishaji wa vifurushi kwa kuwa TPC ina matawi zaidi ya 350 nchi nzima hivyo TPC itasogeza huduma kwa wananchi

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladslaus Matindi amesema kuwa tukio hili ni kubwa kwa ATCL kwa kuwa wameangalia namna mpya ya kufanya biashara na TPC na kutumia fursa hii kwa kuwa TPC ni Shirika pekee lenye mtandao mpana mpaka vijijini ambao ni sawa na ilivyo vituo vya afya na shule zilivyo kila mahali na fursa hii itawanufaisha wote ATCL na TPC kwa kuwa kwa sasa dunia ni kama Kijiji.