Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAWEKA MSUKUMO MPYA SEKTA YA MAWASILIANO


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), Serikali itaendelea kuwekeza katika Sekta ya Mawasiliano ili kuhakikisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kidijitali yanafikiwa na Wananchi wote.

Waziri Kairuki alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya Kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli katika Taasisi zilizo chini ya wizara zilizopo Zanzibar.

Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea TCRA, Shirika la Posta Tanzania, UCSAF na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ambapo alitoa maelekezo mbalimbali ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, hususani katika shehia na visiwa vidogo ambavyo bado vinakabiliwa na changamoto.

Mhe. Kairuki aliielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza ufuatiliaji kwa watoa huduma na kuhakikisha maeneo yote yanapata huduma stahiki za mawasiliano. Na kuwataka kuongeza ushirikiano wa karibu na UCSAF katika kufanikisha ujenzi wa minara kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.

Alipotembelea PDPC, Waziri Kairuki alibainisha umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi na kuagiza Tume kushirikiana na nchi rafiki pamoja na Mahakama ili kuwa na sheria wezeshi zinazolinda haki za wananchi.