Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KUIMARISHA BIASHARA MTANDAO


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma

Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutunga Sheria, kuhakikisha Biashara za Mtandaoni zinasimamiwa ipasavyo, ili kulinda wananchi na watumiaji wengine.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo tarehe 26 Juni, 2024 Bungeni jijini Dodoma, na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Husna Juma Sekiboko (Mb) aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kusimamia biashara ya mtandaoni.

Mhandisi Mahundi amesema, tayari Serikali imetunga sheria mbalimbali za usalama wa mtandao, zikiwemo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya Mwaka 2015, na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022.

Amesema, lengo la Serikali kutunga sheria hizo za usalama wa mtandao ni kuhakikisha kunakuwa na anga salama ya mtandao, na mazingira mazuri ya kuwalinda watumiaji wa mitandao.

Mhandisi Mahundi amesema, pia Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya Mwaka 2015 pamoja na kuandaa Kanuni za Watoa Huduma za Uidhinishaji, ili kuwezesha matumizi ya Saini za Kielektroniki, ikilenga kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa mtandao na usimamizi mahiri wa biashara mtandaoni.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo kuhusu maaandalizi ya Serikali kukusanya mapato kupitia biashara ya mtandaoni, Mhandisi Mahundi amesema, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na wadau wengine, inaandaa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali 2024-2034.

Amebainisha kwamba mkakati huu utaweka mazingira mazuri ya biashara mtandaoni, yanayozingatia ulinzi, usalama na faragha za watumiaji wote wa bidhaa na huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mhandisi Mahundi amesema, Serikali pia inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016 ili kuimarisha mazingira ya matumizi ya teknolojia zinazoibukia katika utoaji wa huduma mbalimbali kidijitali ikiwemo biashara mtandaoni.

Aidha, amesema, Wizara inashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, kukamilisha Mkakati wa Taifa wa Biashara Mtandao, utakaoimarisha biashara ya mtandaoni nchini.