Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAWATAKA WATAALAM WA TEHAMA KUFIKISHA TANZANIA TUNAKOTAKA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na wataalam mbalimbali wa TEHAMA nchini wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau cha kutathmini mahitaji ya taaluma ya TEHAMA yatakayotekelezwa kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika katika ukumbi wa SG Premium Resort,  jijini Arusha Leo Januari 25, 2022.

Na Prisca Ulomi, WHMTH, Arusha

Serikali inawataka wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini kuifikisha nchi ya Tanzania kwenye ngazi inayostahiki ya TEHAMA ili kwenda sambamba na ukuaji na mabadiliko ya TEHAMA nchini ili TEHAMA iwe msingi wa maendeleo ya taifa letu

Hayo yameelezwa na Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua kikao cha kutathmini mahitaji ya taaluma ya TEHAMA nchini kilichofanyika jijini Arusha ambapo kikao hicho kimewakutanisha Wakurugenzi wa TEHAMA na Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara zote nchi nzima ili kwa pamoja waweze kiujadiliana na kuibua mahitaji ya taaluma hiyo Serikalini

“Wakurugenzi mliopo hapa ni vema mtambue vipaji na kuviendeleza kwa kuwa dunia imebadilika, tuwatumie watumishi waliopo Serikalini na kuwaendeleza ili wafikishe nchi tunapohitaji na kuhakikisha wanakuwa wabunifu,” amesisitiza Dkt. Yonazi

Amesema kuwa Wizara hii imepewa dhamana ya kusimamia TEHAMA nchini, hivyo utekelezaji wa majukumu yetu mahali pa kazi lazima TEHAMA itumike kwa maendeleo ya taifa letu kwa kuwa Serikali inatumia TEHAMA kuhudumia wananchi; wananchi wanawasiliana baina yao; inarahisisha shughuli za kiuchumi, kijamii na utawala; na inatumika katika kutoa na kupata huduma mbali mbali bila mtu kulazimika kusafiri kama vile kupata huduma za kibenki; kulipia maji, umeme, bima, leseni; huduma mtandao za afya, elimu

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa mafunzo haya yatatolewa kwa wataalam wa TEHAMA 500 na wataalam wa kada nyingine ili kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanapatiwa mafunzo ya msingi ya TEHAMA kwa kuwa wakati mwingine unakuta kompyuta tu imezimika ila mtumishi haelewi namna ya kuiwasha, hivyo ni muhimu kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma

Naye Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Honest Njau amesema kuwa mafunzo hayo yanagharamiwa na Mradi huo ambao utadumu kwa kipindi cha miaka mitano na unaratibiwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine mradi huu utaongeza nguvu ya minara ya mawasiliano kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G/4G; utafanikisha ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA nchini; ujenzi wa minara 400 ya mawasiliano kwenye maeneo ya kimkakati na kufanikisha uchumi wa kidijitali ambapo mradi wote una gharama ya shilingi bilioni 349

Mkurugenzi wa Utumishi na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Teddy Njau amesema kuwa Wakurugenzi hao wamepewa muda wa wiki mbili wa kuchambua, kubaini na kuwasilisha aina ya mafunzo ya TEHAMA ya kuongeza weledi na ujuzi na kuwasilisha Wizarani ili wataalam hao waweze kupatiwa mafunzo yatakayoifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kidijitali na wataalam hao waweze kutumika ndani ya Serikali; nchini na nje ya nchi.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya washiriki wengine, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Emma Lyimo amesema kuwa kikao hicho kimewafungua na kuwajengea uelewa wa kutathmini mahitaji ya wataalam wa TEHAMA Serikalini na watajumuisha mafunzo stahiki kwa wataalam hao kwenye mipango ya mafunzo ya Wizara zao