Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAWATAKA WASAFIRISHAJI KUUNGANISHA MIFUMO YA UFUATILIAJI WA VIFURUSHI


Na Mwandishi Wetu

Serikali imewataka watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na huduma za haraka kujisajili na kuunganisha mifumo yao na mifumo ya kitaifa ya ufuatiliaji na ubadilishanaji wa taarifa, ili kuwawezesha wateja kufahamu mahali nyaraka na vifurushi vyao vilipo katika kila hatua ya safari.

Wito huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb) wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani 2026. Amesema mifumo ya ufuatiliaji wa vifurushi (Tracking and Tracing) ni muhimu katika kuimarisha uwazi, usalama na ufanisi wa huduma za posta nchini.

Dkt. Mkama amewahimiza watoa huduma ambao bado hawajaunganisha mifumo yao kufanya hivyo, akieleza kuwa ushirikiano na ubadilishanaji wa taarifa ni msingi wa kujenga mtandao jumuishi wa posta unaotoa huduma bora kwa wananchi na wafanyabiashara, huku ukilinda faragha na taarifa za wateja.

Aidha, amezipongeza kampuni za usafirishaji wa haraka zilizoanza kuunganisha mifumo yao na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mawasiliano (Communication Monitoring System – CMS) unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya wadau kutumia teknolojia kuboresha huduma za posta.

Ameeleza kuwa sekta ya posta inaendelea kubadilika kutokana na ukuaji wa biashara mtandao na ongezeko la mahitaji ya huduma za haraka, salama, nafuu na zinazofikika. Ameongeza kuwa mifumo iliyounganishwa itasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kufikia masoko mapya, kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mkama amelitaka Shirika la Posta Tanzania pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuandaa Wiki ya Posta kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani mwaka 2027 kwa ukubwa, ili kutoa fursa kwa kuelimisha umma kwa Wananchi wengi zaidi kuhusu huduma za posta na mchango wake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.