Habari
Serikali Yaunganisha Nguvu Kuendeleza Uchumi wa Kidijitali Tanzania Bara na Zanzibar
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Zanzibar
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdullah, tarehe 27 Januari, 2026 amekutana na uongozi wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya wizara hizo mbili katika kutekeleza masuala mbalimbali ya Sekta ya Mawasiliano na TEHAMA.
Katika kikao hicho, Bw. Abdullah aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Nicholas Mkapa, pamoja na menejimenti ya wizara hiyo na kupokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Bi. Fatuma Mbarouk Khamis, akiwa na menejimenti ya wizara hiyo.
Katika Mkutano huo, wataalamu walifanya mawasilisho kuhusu muundo na majukumu ya wizara hizo, utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) pamoja na mifumo mbalimbali ya kidijitali iliyojengwa na inayoendelea kujengwa.
Baada ya mawasilisho hayo, majadiliano yaliyolenga kubadilishana uzoefu yalifanyika baina ya wizara hizo mbili kwa lengo la kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inaleta manufaa chanya kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Bw. Abdullah alitumia mkutano huo kumkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Zanzibar kushiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Februari 5 hadi 8, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
