Habari
SERIKALI YAUNDA KIKOSI KAZI KUKABILIANA NA UHALIFU WA MITANDAO

Na Grace Semfuko, Maelezo
Serikali imesema inaunda kikosi kazi cha kushughulikia masuala ya uhalifu wa kimtandao, na kuweka mazingira salama kwa wananchi ambao wamekuwa wakikabiliwa na uhalifu huo, ambao unaathiri shughuli zao za kiuchumi.
Kuundwa kwa kikosi kazi hicho ni sehemu ya maazimio ya kikao cha usalama wa mitandao, kilichowakutanisha mawaziri wawili akiwepo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni (Mb) pamoja na wadau wa kisekta na watoa huduma za Mawasiliano, ambao wamesema kuundwa kwa kikosi kazi hicho kutasaidia kuondokana na uhalifu huo.
Akizungumza wakati akitoa maazimio ya kikao hicho, Waziri Masauni amesema kikosi kazi hicho kitahusisha wadau mbalimbali zikiwepo Wizara, Taasisi pamoja na wadau wengine wanaoshughulika na masuala ya uhalifu wa mitandao.
“Tumeamua kuunda kikosi kazi cha kukabiliana na uhalifu wa mtandao ambacho kitashirikisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali za serikali, hususan wizara zetu mbili, ili kwa pamoja tuweze kushughulikia uhalifu huu ambao umekuwa ukiathiri wananchi wengi, watu wamekuwa wakitapeliwa, wakipoteza fedha zao walizozitafuta kwa jasho na watu wachache tu ambao wanataka kujitajirisha kwa kupata kipato cha haraka haraka kwa njia haramu," amesema Mhe. Masauni.
Amesema Jeshi la Polisi limefanya kazi kwa kadiri linavyoweza kushughulikia jambo hili lakini anaamini wadau wote wakifanya kazi kwa kushirikiana wanaweza kufanikiwa kukabiliana na changamoto hiyo kwa haraka zaidi, na ikaweza kuwa na tija zaidi, amesema Mhe. Masauni.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema, ili kukabiliana na uhalifu huo Wananchi wanapaswa kutoa taarifa inapotokea kuna uhalifu huo.
“Inapotokea tukio la uhalifu wa kimtandao kama vile utapeli au ulaghai wananchi tunawasisitiza kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilicho karibu na wewe, kwa hatua zaidi za kijinai, hakuna tukio la kiuhalifu litaweza kufanyiwa kazi kama sio mwananchi mwenyewe kwenda kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi na baadae kuweza kusaidia Jeshi la Polisi kwenye uchunguzi na baadae kusaidia Mkurugenzi wa Mashtaka kwenye Ushahidi mahakamani,” amesema Mhe. Silaa.
Aidha amewataka wananchi wasitoe nywila (password) zao kwa watu wengine wanaowapigia simu kwani kumeibuka wimbi la matapeli suala ambalo linashughulikiwa na serikali kupitia wizara hizo.
“Tumekubaliana na kila mdau ana wajibu wake na mdau wa kwanza ni mwananchi, wizara inatoa wito kwa wananchi kuhakiki namba zao zilizosajiliwa kwa kutumia NIDA zao wizara kupitia TCRA imetoa namba ambayo ni *106# ambayo kila mwananchi anaweza kuingiza kwenye simu yake na kukagua namba yake ya NIDA imetumiwa kwenye usajili wa namba ngapi ili kujua kama kuna namba ambazo zimesajiliwa kwa NIDA yake na hazitumii yeye bali zinatumika kwa usajili wa namba za wahalifu wa kimtandao na akifanya hivyo ataripoti na TCRA wataziondosha namba hizo kwenye usajili” amesema Mhe. Silaa