Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YATOA WITO KUIMARISHA USALAMA MTANDAONI KATIKA ZAMA ZA AKILI UNDE


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dodoma

Serikali imewataka wananchi kuimarisha usalama mtandaoni na kufanya machaguo salama katika matumizi ya teknolojia, hususan katika kuwalinda watoto, katika kipindi hiki cha maendeleo ya kasi ya akili unde na uchumi wa kidijitali.

Wito huo umetolewa leo Februari 10, 2026, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholous Merinyo Mkapa, aliyemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb) katika Maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na kaulimbiu isemayo “Teknolojia Mahiri, Machaguo Salama: Tuwalinde Watoto katika Zama za Akili Unde,” ililenga kuhamasisha jamii kuchukua tahadhari dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo salama ya teknolojia za kisasa, hususan Akili Unde (AI).

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Bw. Mkapa alisema kuwa licha ya Tanzania kupiga hatua kubwa na kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika masuala ya usalama mtandaoni barani Afrika Mashariki na Kati, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa pamoja, ikiwemo uhalifu mtandaoni, ukiukwaji wa faragha, na ulaghai wa kidijitali.

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuboresha mifumo ya kisheria, kuimarisha usalama wa taarifa, na kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha matumizi salama na yenye tija ya teknolojia.

Bw. Mkapa pia alipongeza juhudi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuendesha programu za uhamasishaji, kuanzisha vilabu vya kidijitali, na kushirikiana na taasisi za elimu katika kukuza uelewa wa usalama mtandaoni kwa vijana na wanafunzi.

Alisisitiza kuwa ulinzi wa watoto na usalama mtandaoni kwa ujumla ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wazazi, wadau wa sekta binafsi, na jamii kwa ujumla.