Habari
Serikali Yatoa Maagizo kuhusu Usajili wa Wakusanyaji, Wachakataji na Watunza Taarifa Binafsi
Na Mwandishi Wetu WMTH, Arusha
Serikali imetoa kipindi cha nyongeza cha miezi mitatu, kuanzia leo tarehe 8 Januari 2026, kwa ajili ya usajili wa hiari kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi ambazo bado hazijakamilisha usajili wao. Kipindi hiki ni fursa kwa taasisi hizo kujirekebisha bila kuchukuliwa hatua za kisheria, kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 pamoja na Kanuni zake.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), wakati akifunga Mafunzo Maalum kwa Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi leo tarehe 8 Januari, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Aidha, Waziri Kairuki ameielekeza Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuanza mara moja maandalizi na utekelezaji wa ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria (Compliance Audits). Ameeleza kuwa, endapo ukaguzi huo utabaini taasisi, kampuni au watu binafsi wanaoendelea kukusanya, kuhifadhi au kuchakata taarifa binafsi bila kujisajili, au kinyume na matakwa ya Sheria na Kanuni zake, hatua za kisheria zitachukuliwa bila kusita.
“Baada ya kipindi cha miezi mitatu kumalizika, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi itatekelezwa kikamilifu bila msamaha wowote. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kukiuka Sheria. Hili ni agizo la Serikali na ni sehemu ya msimamo wake wa kulinda haki za kikatiba za wananchi katika uchumi wa kidijitali,” alisema Waziri Kairuki.
Ameongeza kuwa maelekezo hayo yanaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi wa kidijitali unaoaminika, salama na jumuishi.
“Maendeleo ya kweli hayawezi kujengwa juu ya matumizi mabaya ya taarifa binafsi au mifumo isiyo salama. Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi mnatakiwa kuwa viongozi wa mabadiliko, washauri wa menejimenti zenu, na wasimamizi wa utekelezaji wa Sheria ndani ya taasisi zenu,” alisisitiza.
Vilevile, Waziri Kairuki amewataka kwa msisitizo Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi waliohitimu leo kutambua kuwa wanawajibika kisheria kuhakikisha elimu ya ulinzi wa taarifa binafsi inatolewa ndani ya taasisi zao kwa namna endelevu na inayopimika.
“Natarajia muwe mfano wa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo wa kweli. Serikali inatarajia kuona matokeo ya mafunzo haya yakitafsiriwa katika vitendo vinavyojenga imani ya wananchi na wadau wetu,” alihitimisha Waziri Kairuki.
