Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Yatenga Shilingi Bilioni 5 Kuwezesha Kampuni Changa Ndani ya Siku 100


Na Mwandishi Wetu, WMTH

Mji wa Serikali Mtumba – Dodoma

 

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanikiwa kutekeleza ahadi tatu (3) kati ya ahadi 13 ilizopewa ndani ya siku 100, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka.

 

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), wakati akitoa taarifa mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais Samia za mafanikio ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita (Muhula wa Pili), katika Mkutano uliofanyika tarehe 04 Februari, 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kairuki alisema kuwa miongoni mwa ahadi zilizotekelezwa ni kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara ndogo, za kati na uendeshaji wa Kampuni Changa (Start-Ups).

 

“Napenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa Mheshimiwa Rais ametekeleza ahadi hii kwa kishindo. Hadi kufikia Januari 2026, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetengewa Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kuwezesha uendeshaji wa Kampuni Changa, ambapo utekelezaji wake umefanyika kwa kushirikisha Wizara saba (7),” alisema Waziri Kairuki.

 

Waziri Kairuki alieleza kuwa kukuza na kuimarika kwa Kampuni Changa kutafungua fursa nyingi za ajira kwa wananchi, ambapo inakadiriwa kuwa kila Kampuni Changa ina uwezo wa kuajiri watu kati ya 7 hadi 10. Mpango huo unatarajiwa kuongeza kipato cha watu binafsi na kaya zao, kuboresha hali ya maisha, kuinua ustawi wa familia na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali kupitia ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

 

Aidha, Waziri Kairuki aliwahimiza vijana wabunifu wa Kitanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwasilisha maombi ya kuwa wanufaika wa fedha hizo ili kukuza bunifu zao na kujiongezea kipato.

 

Alisema kuwa tangazo la kuwasilisha maombi litatolewa kuanzia tarehe 11 Februari, 2026 kupitia mitandao ya kijamii ya Wizara pamoja na Jumuiya za Kampuni Changa, mara baada ya kukamilika kwa maridhiano ya vigezo vitakavyotumika.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema kuwa ndani ya siku 100 za Uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara imeanza maandalizi ya kuanzisha Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA (ICT Startups Development Fund). Mfuko huo unalenga kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa Kampuni Changa ambazo mara nyingi hukosa fursa ya kupata mikopo kutoka benki na taasisi za fedha au wawekezaji wa kawaida.

 

Vilevile, Wizara imekamilisha maandalizi ya rasimu ya Mwongozo Maalum wa Ushiriki wa Kampuni Changa katika Zabuni za Umma, ambapo Kampuni Changa zitakazosajiliwa, kuhakikiwa na kuthibitishwa kupitia mfumo wa JAMII HUNT, zitaunganishwa moja kwa moja na Mfumo wa Manunuzi ya Umma – NEST, ili kushiriki zabuni za sekta ya TEHAMA kama Makundi Maalum kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2023.