Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YASISITIZA UMUHIMU WA ANWANI ZA MAKAZI KATIKA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Songea

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Wilman K. Ndile amesema mfumo wa Anwani za Makazi ni nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao, hususan katika maeneo ya mipakani kama Songea.

“Tunahakiki taarifa za anwani za makazi ili tujuane vizuri, na sisi tunaoishi maeneo ya mipakani tuwe salama zaidi,” alisema Mhe. Ndile Septemba 25, 2025 wakati akifungua mafunzo ya zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea

Ameongeza kuwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa pamoja na watendaji wa kata na mitaa wanapaswa kufuatilia kwa umakini mafunzo yanayotolewa na wataalam wa Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA), kwa kuwa yatasaidia sio tu katika zoezi la uhakiki, bali pia katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Caroline Kanuti akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya zoezi la Uhakiki wa Anwani za Makazi kwa watendaji wa kata, mitaa na wenyeviti wa mitaa katika halmashauri ya Manispaa ya Songea.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Caroline Kanuti, alisema zoezi la uhakiki litafanyika kwa siku 12 katika Manispaa ya Songea likitanguliwa na mafunzo ya siku moja kwa Wenyeviti, na siku mbili kwa Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji. 

Alisema kupitia zoezi hilo, taarifa za wananchi zitaboreshwa, changamoto za majina ya barabara zitatatuliwa na mtiririko wa namba za anwani utaimarishwa ili kupata tija iliyokusudiwa na kuhakikisha mfumo huu unakuwa na taarifa sahihi.

Ameongeza kuwa mpaka sasa zoezi la uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi limeshafanyika kwenye Halmashauri zaidi ya 40 nchini kwa uratibu wa Wizara, na anwani mpya 535,856 zimesajiliwa, jambo linalothibitisha ongezeko la makazi mapya yanayohitaji anwani.” alisema Bi. Kanuti.

Bi. Kanuti amesema hadi sasa Wizara hiyo imeshatoa mafunzo kwa wataalam na watendaji 9,072 na imejipanga kuendelea kujenga uwezo wa wataalam na watendaji katika ngazi zote ili kuhakikisha uendelevu wa mfumo huu. 

Aidha, alihitimisha kwa kueleza kuwa katika zoezi la Songea, timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, wataalam wa Mkoa na Halmashauri, watashirikiana kwa karibu kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa ufanisi.