Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YASISITIZA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI KATIKA UKUAJI WA TEHAMA


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam

 

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuwa itaendelea kuimarisha mifumo na sera zinazolenga kulinda taarifa binafsi sambamba na kuhamasisha taasisi na wananchi kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi, tarehe 29 Juni, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

 

Dkt. Mkama amesema ni muhimu kuhakikisha taarifa binafsi zinalindwa ipasavyo ili zitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa pekee, jambo litakalosaidia kulinda faragha ya wananchi na kuimarisha matumizi salama ya teknolojia za kidijitali.

 

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Mhe. Balozi Adadi Mohamed Rajabu, amesema kongamano hilo ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania ya kujenga mfumo wa kisasa wa usimamizi wa taarifa binafsi unaozingatia haki za binadamu, unaokuza ubunifu wa kidijitali na kujenga mazingira ya kuaminiana kati ya wananchi na wadau wa maendeleo.

 

Balozi Adadi amesisitiza kuwa Bodi anayoiongoza imeendelea kuweka mazingira salama, ya uwazi na yenye kuaminika katika usimamizi wa taarifa binafsi, hususan katika kipindi hiki ambacho matumizi ya teknolojia za kidijitali yanaongezeka kwa kasi.

 

Amesema kongamano hilo linatoa fursa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu bora za kuimarisha faragha na ulinzi wa taarifa binafsi nchini, sambamba na kuendana na maendeleo ya teknolojia duniani.

 

Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi, linalowakutanisha wataalamu mbalimbali wa TEHAMA nchini linafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 29 Juni, 2026 huku likiongozwa na Kaulimbiu isemayo, “Faragha ya Taarifa ni Nguzo: Kupata Mustakabali Jumuishi wa Kidijitali kuelekea Dira 2050”. Aidha, Kongamano hilo linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 01 Julai, 2026.