Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Yasisitiza Ujumuishi wa Kidijitali kwa Wanawake na Vijana


Na Mwandishi Wetu, WMTH-Dar es Salaam

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kifedha na kitaasisi ili kuchochea uvumbuzi unaojenga ajira na kujitegemea kwa Taifa.

 

Waziri Kairuki alitoa kauli hiyo  Januari 19, 2026, akifungua Kongamano la 9 la Mwaka la TEHAMA (TAIC 2026), jijini Dar es Salaam. Na kuelezea furaha yake kuona jukwaa hili likitenga siku ya hii kwa ajili ya wanawake katika TEHAMA. Huku akisema kuwa hatua hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Wanawake na Wasichana wanashiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kidijitali na uvumbuzi wa kiteknolojia.

 

“Wanawake wana mchango mkubwa katika kuendeleza TEHAMA, kuanzisha bunifu, kuongoza taasisi za kidijitali, na kubuni suluhisho zenye athari chanya za kijamii,” alisisitiza Mhe. Kairuki.

 

Waziri Kairuki pia alisisitiza umuhimu wa vijana katika mabadiliko ya kidijitali, huku akieleza kuwa kupitia kampuni changa za TEHAMA (ICT Startups), vijana wetu wana fursa kubwa ya kujiajiri badala ya kuajiriwa.

 

“Ni malengo ya Serikali kuwa kundi hili litambulike, liendelezwe na liungwe mkono kwenye kuboresha ubunifu wao,” alisema Waziri Kairuki.

 

Waziri Kairuki alieleza hatua za kimkakati zinazochukuliwa na Serikali ili kuhakikisha mabadiliko ya kidijitali yanatekelezwa kwa ufanisi. Aliiagiza Tume ya TEHAMA kuimarisha usajili na uendelezaji wa wataalam wa TEHAMA pamoja na kuimarisha mifumo ya kusimamia na kusaidia kampuni changa bunifu za TEHAMA ili bidhaa na huduma zao ziweze kuingia sokoni kwa ufanisi. Aidha, alizitaka Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuhakikisha zinawasilisha taarifa kuhusu mifumo yao ya TEHAMA kwa Wizara, na kuhakikisha mifumo hiyo inavyosomana na mifumo mingine.

 

Waziri Kairuki alisisitiza pia umuhimu wa wabunifu na waandaaji wa maudhui (“Content Creators”) kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi ya mifumo na teknolojia zinazoibukia, kama vile Akili Unde (AI), ili kuepuka matumizi yanayokiuka maadili ya nchi yetu.

 

Alieleza kuwa Wizara tayari imeandaa mkakati wa Akili Unde na mwongozo wa matumizi wenye kulinda maadili ya nchi, ili kuhakikisha mabadiliko haya ya kidijitali yanafanikiwa bila kuathiri maadili na ustawi wa jamii.

 

Kongamano la Mwaka la TEHAMA (TAIC 2026) linahimiza kujenga uchumi wa kidijitali unaohusisha kila mtu na kuzingatia haki, ujumuishi, na maendeleo endelevu. Kaulimbiu ya mwaka huu, “Mabadiliko ya Kidijitali Yanayochochea Athari za Kijamii na Uvumbuzi wa Kiteknolojia kwa Taifa lenye Mafanikio, Haki, Ujumuishi na Kujitegemea,” inaakisi dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050, ambayo imejikita katika matumizi ya teknolojia za kidijitali kama nyenzo muhimu za kukuza ujumuishi wa kijamii, uvumbuzi endelevu, na kujitegemea kiuchumi.

 

Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA na imetenga mikakati ya kimkakati ya kuhakikisha kuwa huduma za kidijitali zinawafikia wananchi wote. Hadi kufikia Disemba 2025, Serikali imekamilisha ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano, ambayo inatoa huduma ya mawasiliano kwa wananchi. Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.