Habari
Serikali Yapongezwa Kwa Mageuzi Makubwa Katika Sekta Ya Mawasiliano Nchini
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Arusha
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ambapo alipokelewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. CPA Amos Makala, leo tarehe 9 Januari, 2026, jijini Arusha.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki alipata nafasi ya kueleza maendeleo ya sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (TEHAMA) pamoja na mchango wake katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa mazungumzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makala, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano, akisema kuwa maboresho ya miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo upanuzi wa huduma za intaneti na matumizi ya mifumo ya TEHAMA, yameongeza ufanisi katika shughuli za kiserikali, biashara na huduma za kijamii mkoani humo.
Mhe. Makala alibainisha kuwa maendeleo hayo yamerahisisha utoaji wa huduma katika sekta muhimu kama elimu, afya na biashara, sambamba na kuboresha mazingira ya uwekezaji na maendeleo ya kijamii kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake, Waziri Kairuki alisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma bora, salama, za uhakika na zenye gharama nafuu zinawafikia wananchi wote, hususan waliopo vijijini na maeneo yenye changamoto ya miundombinu.
Aidha, Waziri Kairuki alisema Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa sera, mikakati na miradi ya mawasiliano nchini, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kukusanya maoni yatakayosaidia kuiboresha zaidi sekta hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Waziri Kairuki yuko mkoani Arusha kwa ziara ya Kikazi ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine atatembelea baadhi ya vituo vya wabunifu wa Kampuni Changa za TEHAMA zilizopo mkoani humo.
