Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA SEKTA YA MAWASILIANO


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amekutana na viongozi wa Kampuni ya Helios Towers Tanzania inayojishughulisha na Ujenzi wa Minara ya Mawasiliano hapa nchini.

 

Katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 17 Juni, 2026 viongozi wa Kampuni ya Helios Towers walieleza kuridhishwa kwao na ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka Wizarani pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano nchini.

 

Wakizungumza katika kikao hicho, viongozi hao wamempongeza Waziri Kairuki kwa juhudi na utayari wake wa kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Mawasiliano ambazo zimeongeza ufanisi wa huduma za mawasiliano na kuimarisha imani ya wawekezaji.

 

Aidha, Kampuni ya Helios Towers Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini pamoja na kutekeleza programu mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo ya elimu, afya na maendeleo ya kijamii.

 

Kwa upande wake, Mhe. Kairuki aliishukuru kampuni hiyo kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini na kuhimiza kuendelea kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

 

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea uwekezaji, ubunifu na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wote, hususan katika maeneo ya vijijini na ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu na miundombinu ya mawasiliano.