Habari
SERIKALI YAPOKEA MAONI YA UANZISHWAJI WA CHUO MAHIRI CHA TEHAMA
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Zanzibar
Serikali imeendelea kutekeleza hatua mbalimbali za uanzishwaji wa Chuo Mahiri cha TEHAMA ambapo imekutanisha wadau kwa ajili ya kupokea maoni kuhusu uandaaji wa Sheria ya Uanzishwaji wa Chuo Mahiri cha TEHAMA kitakachokuwa nguzo muhimu ya kukuza maendeleo na weledi wa wataalamu wa TEHAMA nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Bi. Fatuma Mbarouk Khamis, amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa wa Teknolojia ili kukidhi mahitaji ya Taifa ya sasa na ya baadaye.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholas Mkapa, alisema uanzishwaji wa Chuo hiki ni sehemu ya utekelezaji wa Ajenda ya Taifa ya Uchumi wa Kidijitali inayolenga kuongeza ushindani wa Taifa, kuimarisha utoaji wa huduma za Serikali Mtandao na kukuza sekta ya TEHAMA kama mhimili wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Naye Mratibu wa Mradi wa Chuo hicho, Dkt. Ally Simba, amesema kuanzishwa kwa NDTI kutasaidia kuendeleza miradi na mifumo ya kidijitali inayotekelezwa nchini, kujenga uwezo wa wakufunzi wa TEHAMA katika vyuo mbalimbali, pamoja na kuandaa vijana wenye ujuzi wa hali ya juu wa kiteknolojia watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Kwa ujumla, kikao hicho kiliwapa fursa wadau kutoka Zanzibar na Tanzania Bara kutoa maoni yao kuhusu muundo wa Sheria ya NDTI, ili kuhakikisha taasisi hiyo inakuwa jumuishi, shirikishi na inayozingatia maslahi ya Taifa kwa pande zote mbili za Muungano, huku ikitarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
