Habari
Serikali Yaongeza Ufanisi wa Huduma Kupitia Ugawaji wa Kompyuta Zanzibar
Na Mwandishi Wetu, WMTH-Zanzibar
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Ndugu Fatma Mabrouk Hamis, amesema kuwa
Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo jumuishi inayowezesha kubadilishana taarifa kupitia miundombinu ya umma ya kidijitali, ikiwemo mifumo ya utambulisho wa kidijitali, malipo ya kielektroniki, pamoja na mifumo ya kubadilishana taarifa kati ya taasisi za umma.
Ndugu Fatma aliyasema hayo tarehe 13 Aprili, 2026 wakati wa Hafla ya Kukabidhi Vifaa vya TEHAMA (kompyuta) kwa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar. Na kuongeza kuwa vifaa vinavyokabidhiwa leo vitachangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya watumishi wa umma, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika taasisi za Serikali zilizopo Zanzibar.
Ndugu Fatma alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali unaolenga kuhakikisha mageuzi ya kidijitali yanakuwa na tija kwa taifa.
“Ni muhimu vifaa hivi vitumike kwa ufanisi ili kuongeza thamani katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisisitiza Ndugu Fatma.
Aidha, aliwataka watumishi wa umma kutumia vifaa hivyo kwa ubunifu na weledi ili kuharakisha utoaji wa huduma bora, za haraka na zenye kuaminika kwa wananchi. Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza ajenda ya mageuzi ya kidijitali, ikiwemo kubadilishana uzoefu, kuimarisha mifumo ya pamoja na kujenga uwezo wa rasilimali watu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Ndugu Mansoura Kassim aliishukuru Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) kwa kuwapatia vifaa hivyo, akieleza kuwa vitasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma pamoja na kuboresha utendaji wa watumishi katika ofisi hiyo.
Naye Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bakari Mwamgugu, alisema kuwa kupitia mradi huo, jumla ya kompyuta 36 zimetolewa kwa upande wa Zanzibar ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma Serikalini. Alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha mafanikio ya uchumi wa kidijitali pamoja na uchumi wa buluu nchini.
