Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Yaongeza Kasi ya Matumizi ya TEHAMA


Na Mwandishi wetu - WMTH Ukerewe

 

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mhe. Christopher Emily Ngubiagai ameongoza zoezi la ugawaji wa vishikwambi kwa Watendaji wa Kata na Vijiji wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kiutendaji katika ngazi za msingi za utawala.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Ngubiagai amesema kuwa vishikwambi hivyo vitasaidia kuongeza kasi ya utendaji kazi kwa watendaji wa kata na vijiji, hususan katika ukusanyaji, uhifadhi na usimamizi wa taarifa mbalimbali zinazohitajika kwa maendeleo ya wananchi.

 

Vilevile, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika matumizi ya TEHAMA ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa haraka, ufanisi na kwa gharama nafuu.

 

Mhe. Ngubiagai amewataka watendaji wote waliopokea vifaa hivyo kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuvitunza ipasavyo huku akitoa angalizo kuwa matumizi mabaya ya vishikwambi hivyo yanaweza kuleta madhara makubwa kwa Serikali na wananchi, ikiwemo kupotea kwa taarifa muhimu na kuathiri utoaji wa huduma.

 

Watendaji hao pia walikumbushwa kuwa nidhamu, uwajibikaji na uzalendo ni misingi muhimu katika matumizi ya rasilimali za umma.

 

Sambamba na zoezi hilo, wataalamu wa NaPA wamewajengea uwezo Watendaji wa Kata na Vijiji kuhusu matumizi sahihi ya vifaa hivyo.

 

Mafunzo hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika utawala wa umma. Watendaji wa kata na vijiji wanatarajiwa kutumia maarifa na vifaa walivyopatiwa kuboresha huduma kwa wananchi, kuongeza uwazi katika utendaji kazi na kuimarisha ukusanyaji wa taarifa muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya ya Ukerewe na Taifa kwa ujumla.