Habari
Serikali Yalenga Kuunganisha Mifumo ya Kidijitali kuimarisha Huduma za Maji nchini
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dodoma.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amefanya ziara katika Ofisi za Wizara ya Maji zilizopo Mtumba, jijini Dodoma kwa lengo la kujadili kwa pamoja namna mifumo ya usimamizi kupitia Teknolojia za Kisasa itakavyoleta mageuzi na kuchochea uchumi wa kidijitali kwenye Sekta ya Maji nchini.
Katika ziara hiyo, iliyofanyika tarehe 02 Februari, 2026 Mhe. Kairuki alipokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), na baadae kufanya mazungumzo ya kina kuhusu namna bora ya kushirikiana katika kujenga mifumo ya TEHAMA itakayorahisisha utoaji wa huduma za maji kwa wananchi.
Waziri Kairuki alitaja lengo la ziara hiyo kuwa ni kuona namna Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itakavyoiwezesha Wizara ya Maji katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maji kidijitali inayosimamia ukusanyaji wa takwimu, usimamizi wa miradi na ufuatiliaji wa huduma za maji nchini.
Akizungumza katika kikao hicho,
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), alieleza utayari wa wizara hiyo kushirikiana kikamilifu na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika ujenzi wa mifumo hiyo kwa kutumia teknolojia za kisasa pamoja na kuwezesha wataalam wa ndani ili kuboresha utoaji wa huduma za maji na kuongeza mapato.
Katika kikao hicho Mawaziri hao wawili waliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), Makatibu Wakuu, Menejimenti za Wizara zote mbili pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba.
Ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uratibu wa wizara mbalimbali katika kutekeleza mageuzi ya kidijitali, kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa utoaji wa huduma za kijamii katika sekta ya maji nchini.
