Habari
SERIKALI YAITAKA SEKTA BINAFSI KUSHIRIKIANA MATUMIZI BORA YA AKILI MNEMBA

Mwandishi Wetu- WHMTH, Dar es Salaam
Wito umetolewa kwa Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu, na Mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha vizazi vijavyo vinaandaliwa ipasavyo kwa uchumi wa Akili Mnemba (Artificial intelligence-AI).
Wito huo umetolewa leo tarehe 26 Septemba, 2024 jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) wakati akifungua Kongamano la Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT).
Lengo la kongamano hilo ni kuwaweka pamoja wanachama wa IoDT, Viongozi wa kampuni na biashara, Maafisa wa Umma na wadau wengine kupata jukwaa la pamoja la kujifunza, kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu mada mtambuka na muhimu katika majukumu yao ya kila siku.
Mhandisi Mahundi amesema, Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kunakuwa na matumizi bora ya teknolojia za AI ili kuboresha maisha ya Watanzania na kuimarisha uchumi wa nchi.
"Tunahitaji kuwekeza katika mafunzo ya kitaaluma na kujenga uwezo wa wafanyakazi wetu ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufaidika na mapinduzi haya ya kidijitali,” amesema Mhandisi Mahundi na kuongeza;
“Ni matumaini yangu kuwa matokeo ya tukio la leo yatatusaidia kuweka msingi mzuri wa uongozi wa kidijitali nchini na kwa pamoja, tunaweza kufanya mabadiliko haya ya kidijitali".
Amesisitiza kwamba, Serikali kwa kushirikiana na wadau wote itahakikisha yanafanyika mabadiliko hayo ya kidijitali ili yawe kichocheo cha maendeleo endelevu na ustawi wa taifa zima.