Habari
Serikali Yaipongeza Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa Mchango wake katika Uchumi wa Kidijitali
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema Serikali imelenga kupanua miundombinu ya mawasiliano mijini na vijijini, kuhakikisha huduma bora na nafuu, pamoja na kukuza ubunifu na matumizi ya TEHAMA katika sekta zote.
Waziri Kairuki ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Makao Makuu ya Kampuni ya Vodacom Tanzania iliyofanyika tarehe 13 Februari, 2026 jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki alieleza kuwa Sekta ya Mawasiliano imeendelea kuwa ni mhimili muhimu wa uchumi wa kidijitali na maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na menejimenti ya kampuni hiyo, Waziri Kairuki alisema ziara yake imelenga kupata uelewa wa kina kuhusu shughuli za uendeshaji, mikakati ya upanuzi wa mtandao, uwekezaji katika teknolojia za kisasa pamoja na changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Tanzania ya kuwa taifa lenye uchumi wa kidijitali jumuishi ifikapo mwaka 2030 na kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri Kairuki aliipongeza Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kuongoza kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini kupitia ruzuku ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambapo imefanikiwa kujenga na kuboresha minara kwa mujibu wa makubaliano na Serikali. Na kusisitiza kuwa mafanikio hayo yana mchango mkubwa katika kuongeza ujumuishaji wa kifedha, kukuza biashara na kuimarisha ajira nchini.
Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na Kampuni ya Vodacom Tanzania kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji, kupunguza gharama za uendeshaji na kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu.
