Habari
SERIKALI YAIHAKIKISHA TBC KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI ILI IWEZE KUTEKELEZA DHIMA YAKE KWA UMMA

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma
Serikali imelihakikishia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwamba inafanya kila linalowezekana kuhakikisha shirika hilo linatekeleza majukumu yake muda wote, na itaendelea kutatua na hatimaye kumaliza changamoto zote zinazolikabili, zikiwemo za kifedha, vifaa na rasilimali watu.
Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa tarehe 20 Septemba, 2024 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) wakati akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage (Hazina) jijini Dodoma.
"Naomba niwahakikishie kuwa Serikali inafanya kila linalowezekana ili TBC itekeleze majukumu yake muda wote, na Wizara itahakikisha changamoto zote zinazowakabili zinatatuliwa kwa wakati kwani Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha mnawezeshwa kifedha, vifaa na rasilimali watu ili kutekeleza dhima yake kwa umma wa Watanzania ", alisema Mhe. Silaa.
Mhe. Silaa amesema, Serikali inatambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na TBC kuhakikisha kunakuwa na fedha za kutosha na kwamba kwa kutambua changamoto za kifedha kwa Shirika, Wizara inasimamia kwa karibu mchakato wa kutungwa kwa Sheria ya TBC, ambayo pamoja na mambo mengine, itaiwezesha kupata vyanzo vya mapato vya uhakika, endelevu na toshelevu.
"Waraka wa Sheria hii umeshasomwa kwa mara ya kwanza Bungeni na hatua inayofuata ni kupitishwa na Bunge baada ya kupata maoni ya wadau kama taratibu zinavyoelekeza" amesema Mhe. Silaa.
Aidha, ameipongeza TBC kwa maendeleo makubwa yaliyofikiwa ya kufunga mifumo ya TEHAMA katika miundombinu ya studio za redio na televisheni, upanuzi wa usikivu uliofikia asilimia 92 mwaka huu, na maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya TBC eneo la Vikonje Dodoma uliofikia asilimia 26 hadi sasa.
Awali akimkaribisha Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Bw. Stephen Kagaigai amewashauri watanzania kufuatilia maudhui yanayotolewa na Shirika hilo kwani ndicho chombo cha Umma wa Watanzania.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt. Ayub Rioba Chacha ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa unaowezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa licha ya changamoto ndogo ndogo ikiwemo ya upungufu wa watumishi wenye ujuzi na wazoefu ambao wengi sasa wamefikia umri wa kustaafu.