Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Yahimiza Ushiriki wa Wasichana katika Mapinduzi ya Kidijitali


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb) amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji binafsi na matumizi sahihi ya teknolojia katika kujenga jamii yenye mawasiliano salama, jumuishi na yenye tija kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Akizungumza katika maadhimisho ya kuhamasisha ushiriki wa wasichana katika masuala ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), Dkt. Mkama alisema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imeendelea kuwa nyenzo muhimu inayowezesha sekta mbalimbali kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, urahisi na haraka, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

 

Alisema pamoja na mchango huo, kasi ya mabadiliko ya teknolojia inalazimu Serikali kuweka mifumo thabiti ya kisera, kisheria, kimkakati na kitaasisi ili kuendana na maendeleo ya TEHAMA duniani.

 

Alibainisha kuwa ukosefu wa usawa wa kijinsia katika masuala ya Sayansi na Teknolojia umechangia wasichana wengi kukosa fursa za ajira zinazohitaji ujuzi wa TEHAMA na kusisitiza umuhimu wa kuhamasisha wanawake na wasichana kusoma masomo ya TEHAMA ili kupunguza pengo la kijinsia, kuongeza ajira, kukuza uchumi wa Taifa na kulinda haki na usawa.

 

Aidha, alieleza kufurahishwa kwake na ushiriki wa wasichana kutoka ngazi mbalimbali za elimu, wakiwemo wenye mahitaji maalum kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya kidijitali.

“Wito wangu kwa viongozi wa shule na vyuo kuhakikisha wanaanzisha klabu za kidijitali ili kuwajengea vijana uwezo wa ubunifu na ushindani katika soko la ajira la kimataifa.”

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Nicholaus Mkapa alisema maadhimisho hayo yana umuhimu mkubwa kwa mtoto wa kike ambao kwa muda mrefu kumekuwa na uwakilishi mdogo wa wanawake.

“Pia ni katika kukuza usawa wa kijinsia katika teknolojia kwa kuwajengea wasichana kujiamini na kuchagua taaluma za TEHAMA, na kuhamasisha ujifunzaji wa masomo ya sayansi na teknolojia kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu.”

 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso alishauri Serikali kusimamia maudhui ili kudhibiti matendo ambayo si mazuri kwa taifa ikiwa ni njia ya kunusuru Kundi la vijana wasiingie kwenye mfumo ambao utawafanya watanzana kuiga vitu ambavyo havitakuwa na faida kwa taifa.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari alisema maadhimisho hayo yametanguliwa na mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyohusisha jumla ya washiriki 281 kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu, yakilenga kuwajengea uwezo katika teknolojia zinazoibukia.

 

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda alisema katika kuhamaisha ujifunzaji TEHAMA kwa kuziwezesha shule kupata kompyua katika shule 1,021 na kuwajengea uwezo walimu shule za sekondari za umma na kuwafikia walimu 4470.