Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAENDELEA KUTOA ELIMU JUU YA USALAMA WA MTANDAO JIJINI ARUSHA


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Arusha 

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea na kampeni ya kutoa elimu juu ya usalama wa mtandao katika shule mbalimbali jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwezi wa Usalama wa Mtandao Duniani.

Bw. Hafidhi Masoud, mmoja wa wataalamu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alizungumzia tabia hatarishi ambazo watu hufanya wakiwa mtandaoni, zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kufanyiwa uhalifu wa mtandaoni. Alieleza kuwa watu wengi hutoa taarifa binafsi kama majina kamili, mahali walipo, picha, na tarehe ya kuzaliwa, bila kujua kuwa taarifa hizo zinaweza kutumiwa vibaya.

Aidha, Bw. Masoud alikemea tabia ya kupuuza tahadhari za kiusalama kama kusasisha (update) programu na simu zao mara kwa mara, jambo ambalo linawaweka katika hatari zaidi. Na kusisitiza mbinu mbalimbali ambazo mtu anaweza kuzitumia kujilinda anapokuwa mtandaoni, ikiwa ni pamoja na kuwa na nenosiri thabiti, kutoaminiana kiholela na kuepuka kubonyeza viungo visivyo sahihi.

Kwa upande wake, Bw. Venance Mwanjabike alifafanua juu ya aina za uhalifu wa kimtandao ambazo zimeendelea kushamiri nchini, ikiwemo hadaa (phishing), wizi wa akaunti, na utapeli wa kifedha. Alieleza kwa kina jinsi wananchi wanaweza kujiepusha na aina hizo za uhalifu, na pia namna ya kuripoti matukio hayo kwa mamlaka husika.

Bw. Bukori Bukori Afisa TEHAMA kutoka wizarani,  elimu kuhusu hatua ambazo taasisi binafsi na wananchi wanapaswa kuchukua ili kujikinga na uhalifu wa mtandaoni. Alisisitiza umuhimu wa kuwa na sera za usalama wa mtandao katika taasisi, kuwaelimisha watumishi na wananchi kuhusu hatari za kimtandao, pamoja na kuripoti matukio ya uhalifu mara yanapotokea.

Wakati huo huo, Kaimu Afisa Elimu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Bw. Charles Nyatadu Mwita, alitoa shukrani kwa wataalamu kutoka wizara kwa kuwatembelea na kutoa elimu hiyo muhimu kwa walimu na wanafunzi. Alieleza kuwa elimu hiyo ni ya msingi sana kwa maisha ya sasa na ya baadaye, na akaisihi jamii ya walimu na wanafunzi kuzingatia mafunzo waliyopata ili kujilinda dhidi ya vitisho vya kimtandao.