Habari
SERIKALI YAENDELEA KUKUZA USHIRIKI WA WASICHANA KATIKA TEHAMA
Na Mwandishi wetu, WMTH - Mbeya
Afisa TEHAMA Mkuu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Asia Abdallah, amesema Serikali imeendelea kuwajengea uwezo Wasichana katika matumizi ya teknolojia ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Ndugu Asia Abdallah ameyasema hayo wakati akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Mifumo, Huduma za TEHAMA na Uzingatiaji, Bw. Mohammed Mashaka, katika ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa Wanafunzi wa Kike walioko katika Shule za Sekondari yanayoendelea katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya TEHAMA kwa Mtoto wa Kike kwa mwaka 2026.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wanafunzi wa kike kutoka shule za sekondari katika Mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Iringa, Njombe na Ruvuma, yakilenga kuwapa ujuzi wa vitendo katika nyanja mbalimbali za TEHAMA.
Kupitia mafunzo hayo, wanafunzi wanatarajia kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo matumizi ya Kompyuta, ubunifu wa kidijitali na urushaji wa ndege nyuki (Drones), jambo linalochochea hamasa ya wasichana kujiamini na kuvutiwa zaidi na masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
Siku ya Kimataifa ya TEHAMA kwa Mtoto wa Kike huadhimishwa siku ya Alhamisi ya nne ya mwezi Aprili ya kila mwaka ambapo mwaka huu itafanyika Aprili 23, 2026 jijini Dodoma ikiwa na kaulimbiu “Akili Unde kwa Maendeleo: Wasichana Wakichagiza Mustakabali wa Kidijitali” (AI for Development: Girls Shaping the Digital Future).
