Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YADHAMIRIA KILA MTANZANIA KUWA NA ANWANI YA MAKAZI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akizungumza kuhusu aina mbalimbali za vibao vya anwani za makazi wakati wa semina ya kuwajengea uelewa Makatibu Tawala wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara kuhusu utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi iliyofanyika Oktoba 21, 2021 jijini Dodoma.

 

DODOMA

* RAS Wote Simamieni Utekelezaji wa Anwani za Makazi kwenye Maeneo Yenu

Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anakuwa na anwani za makazi ifikapo mwaka 2022.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.  Zainab Chaula katika semina ya kujenga uelewa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara kuhusu utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi.

"Tunatarajia kufikisha mawasiliano mpaka vijijini, tunataka nchi nzima iwe na anwani ya makazi," amedokeza Dkt. Chaula.

Aidha, amehabarisha kuwa baadhi ya faida za kuwa anwani za makazi ni kurahisisha ukusanyaji kodi, kuwezesha biashara mtandao na kuimarisha ulinzi na usalama.

Awali, akifungua semina hiyo, Katibu Mkuu wa  Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali za Mikoa zina majukumu ya kusimamia utekelezaji wa anwani za Makazi kwenye maeneo yao 

"Serikali yetu ya Tanzania kupitia Sera ya Posta ya mwaka 2003 imeimarisha mifumo ya anwani za makazi inayoundwa na barabara, njia na namba za nyumba," amebainisha.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo amesisitiza ushirikiano ili kufikia malengo kwa kuwa moja ya manufaa ya anwani hizo ni kuwezesha na kufanikisha utambuzi wa majengo na viwanja vilivyopo ili kurahisisha kazi ya mipango miji na utekelezaji wa majukumu ya kiuchumi na kijamii kwa Serikali na wananchi kwa ujumla

"Naamini tutaendelea kushirikiana katika kujenga nchi yetu na kuwahudumia Watanzania," ametanabaisha Bi. Makondo

Ibara ya 61(m) ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 inaielekeza Serikali iliyopo madarakani kuhakikisha anuani za makazi zinawekwa nchini ili kurahisisha upatikanaji, utoaji na ufikishishaji wa huduma mbali mbali kwa wananchi