Habari
MAPITIO YA MKAKATI WA UMOJA WA POSTA AFRIKA (PAPU) WAONESHA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA SEKTA YA POSTA AFRIKA.
Na Mwandishi Wetu, WMTH - Kampala, Uganda.
Mapitio ya Mkakati wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) yanaonesha mafanikio makubwa katika kuendeleza sekta ya posta barani Afrika, kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026. Mafanikio hayo yaliwasilishwa katika Mkutano wa 44 wa Baraza la Utawala uliofanyika Kampala, Uganda, ambapo Tanzania ilishiriki kama mwanachama.
Mkakati huo uliopitishwa mwaka 2021 ulilenga kuifanya sekta ya posta kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa kidijitali na ujumuishi wa kijamii, sambamba na kuhamasisha nchi wanachama kuipa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya kitaifa.
Utekelezaji wa mkakati ulizingatia nguzo tano kuu, zikiwemo kuimarisha mazingira wezeshi, sera na mifumo ya kisheria na kiteknolojia, kujenga uwezo wa waendeshaji, kukuza usawa wa kijinsia, na kuboresha utendaji wa Sekretarieti ya PAPU.
Katika utekelezaji huo, kamati nne za PAPU zilisimamia shughuli mbalimbali kwa kushirikiana na wataalam na vikundi kazi, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya mipango iliyopangwa ilifanikiwa kutekelezwa.
Mafanikio hayo yamechochewa na juhudi katika maeneo ya usimamizi wa majanga, ukusanyaji wa michango ya wanachama, pamoja na ubunifu na matumizi ya teknolojia za kidijitali, huku shughuli zilizosalia zikiendelea katika mkakati mpya wa mwaka 2026 hadi 2030.
Tanzania ikiwa moja wa Mwanachama wa PAPU imetuma timu ya wataalam kuhudhuria Mkutano huo ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa.
