Habari
Serikali Yaboresha Huduma za Mawasiliano Jimbo la Lupa
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kuboresha huduma za mawasiliano nchini, ikiwemo katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Lupa. Kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Awamu ya Tisa ya Utekelezaji wa Miradi ya Mawasiliano Vijijini, ujenzi wa mnara wa mawasiliano unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026.
Hayo yameelezwa leo, Juni 5, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zacharia Mkama, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Rukwa, Masache Njelu Kasaka, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Aidha, Dkt. Mkama amesema kuwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulifanya ziara katika kijiji hicho na kujionea maendeleo ya mradi huo. Ameongeza kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi ameahidi kukamilisha ujenzi wa mnara huo ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni 2026, hatua itakayosaidia kutatua changamoto ya mawasiliano iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa kijiji hicho pamoja na maeneo ya jirani.
Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya mawasiliano vijijini ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za mawasiliano na kunufaika na fursa za Uchumi wa Kidijitali.
