Habari
SERIKALI YAANZA MCHAKATO WA KUANDAA MUONGOZO WA TAIFA WA USIMAMIZI WA DATA KIELEKTRONIKI

Na Mwandishi Wetu WMTH-Dodoma
Mkurugenzi wa Uendelezaji Mifumo na Huduma za TEHAMA wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohamed Mashaka, amefungua rasmi warsha ya mafunzo ya usimamizi wa data za kielektroniki inayojumuisha pia ushirikishaji wa wadau kutoka sekta mbalimbali.
Warsha hiyo ililenga kujenga uwezo (capacity building) na kushirikisha wadau katika kujadili na kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya data, sheria na miongozo ya kitaifa na kimataifa inayosimamia data, pamoja na umuhimu wa muunganiko wa mifumo ya TEHAMA ili kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa kielektroniki.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bw. Mashaka alisema, “Masuala ya taarifa (data) ni muhimu kwetu sote, na sisi kama nchi ni lazima tuwe tayari na kuwa washindani kwenye masuala ya utandawazi duniani yanayokwenda kwa kasi.”
Aidha, alisisitiza kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kuandaa mwongozo wa kitaifa wa usimamizi wa data za kielektroniki (National Electronic Data Governance) ili kuhakikisha Tanzania ina mfumo thabiti wa kusimamia na kulinda rasilimali hizo muhimu.
Bw. Mashaka aliongeza kuwa, Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali unaendelea kutekelezwa ili kuchochea matumizi ya TEHAMA katika sekta mbalimbali za uchumi, jambo linaloongeza kasi ya ukuaji wa data za kielektroniki nchini. Data hizo zimeelezwa kuwa rasilimali muhimu katika zama za kidijitali na zinahitaji usimamizi wa kitaifa wenye ufanisi.
Warsha hiyo imeandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA), Idara ya Teknolojia, Ubunifu, Uunganishaji na Miundombinu (TICID), na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ).
Aidha, Warsha ilianza Agosti 26, 2025 jijini Dodoma na inatarajiwa kukamilika Agosti 29, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo wadau kutoka sekta ya umma, binafsi na asasi za kiraia wanashiriki, huku wataalamu wa ndani na nje ya nchi wakitoa ujuzi na uzoefu.
Matokeo ya warsha hii yanatarajiwa kuwa chachu ya kuanza mchakato rasmi wa kuandaa Mwongozo wa kitaifa wa usimamizi wa data za kielektroniki nchini.