Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAANZA KUCHUKUA HATUA KUKOMESHA WIZI MITANDAONI.


Na Mwandishi Wetu, WHMTH 

Serikali imesema tayari imechukua hatua kadhaa ili kuweka mazingira salama kwa wananchi wanaotumia mitandao, ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022.

Lengo kuu kutungwa kwa sheria hiyo ni kuweka utaratibu wa kuhakikisha wakusanya taarifa wote wanafuata misingi ya kulinda taarifa za mwananchi.          

Kauli hiyo imetolewa tarehe 15 Mei, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye wakati akijibu Swali la Mbunge wa Buhigwe Mhe. Kavejuru Felix aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali, kukomesha wizi mitandaoni. 

Waziri Nape amesema, pia Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao chini ya Jeshi la Polisi, kikiwa na jukumu la kufanya uchunguzi wa makosa ya mitandao ikiwemo wizi wa aina yoyote kwenye mtandao, na kuandaa majalada ya mashtaka, kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.  

Amesema, Serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao, lakini pia kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao, na kuchukua hatua stahiki yanapobainika, na kujenga mazingira salama ya kisheria.

Aidha, Waziri Nape amesema, hatua nyingine iliyochukuliwa ni kuanzishwa kwa namba ya kutoa taarifa ya uhalifu mitandaoni, 15040, kushirikiana na Watoa Huduma wa Simu za mkononi.

"Serikali itaendelea kuongeza jitihada za kuelimisha umma namna nzuri ya kutumia TEHAMA ili kuendelea kudhibiti matukio ya utapeli na wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi," ameeleza Waziri Nape.

Amesema, namba inayoripotiwa na kuthibitika kufanya uhalifu kwa kutuma ujumbe au kupiga simu za utapeli hufungiwa, pamoja na kifaa kilichotumika yaani simu, ili kisifanye kazi, na kitambulisho cha NIDA kilichotumiwa kusajili namba husika hufungiwa kusajili.