Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAAHIDI MAZINGIRA BORA KWA WAWEKEZAJI SEKTA YA MAWASILIANO NCHINI


Towerco of Africa Tanzania na British International Investment zasaini makubaliano katika ujenzi wa minara

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), amesisitiza nia ya Serikali kuunga mkono uwekezaji wa sekta binafsi hasa katika sekta ya mawasiliano.

Waziri Nape aliitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi wa minara ya mawasiliano kati ya kampuni ya Towerco of Africa Tanzania na British International Investment. Hafla hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro (Hyatt Regency Hotel), jijini Dar es Salaam.

Waziri Nape alielezea kuwa ujio wa sekta binafsi katika uwekezaji wa mawasiliano ni matokeo ya kupitishwa kwa bajeti ya Serikali, na hivyo anaona ni mafanikio makubwa. 

Waziri Nape pia amezipongeza kampuni hizo mbili kwa makubaliano yao na alitambua kuwa yataongeza nguvu katika harakati za mapinduzi ya nne ya viwanda nchini Tanzania. 

Mhe. Nape ameihakikishia sekta binafsi kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji, ili kuchochea ukuaji wa sekta ya mawasiliano na kukuza uchumi wa nchi.