Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAAHIDI KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI


Na Isabella Katondo, WHMTH, Dodoma

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) ameihakikishia Kamati ya Bunge kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 wizara itaendelea kuongeza kasi katika utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali kama ilivyofanya kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambao hadi Februari, 2024 mradi umeshapokea fedha kwa asilimia 251.

Waziri Nape ametoa ufafanuzi huo, leo Machi 22, 2024 jijini Dodoma wakati akiwasilisha utekelezaji wa mipango na bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 na makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2024/25 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.    

“Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ni mradi ambao ni wa muda mrefu na fedha zake zinatoka nje, hivyo kadri tunavyomaliza ndivyo tunavyopata fedha nyingine, kwa hiyo uwezekani wa kupata fedha zaidi ya milioni 200 upo. Na huku ndipo ilipo miradi ile ya miradi ya minara, ni matumaini yangu kuwa kwa kasi tunayoendelea nayo inawezekana hata mwakani hali ikawa ni hivyo”, alisema Waziri Nape.

Sambamba na hilo, Waziri Nape ameieleza Kamati ya Bunge kuwa kabla ya kuwasilisha bajeti ya wizara bungeni, wizara imejipanga kufanya operesheni ya uhakiki wa Anwani za Makazi. Na kimsingi zoezi hili litahitaji hela zaidi lakini kwa bahati nzuri Serikali ya Jamhuri ya Korea tayari imekubali kutupa fesha kiasi cha dola za kimarekani shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuboresha anwani za makazi 


Waziri Nape ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa usimamizi mzuri na miongozo ambayo imekuwa ikiitoa kwa wizara na pongezi ilizozitoa kwa Taasisi za TCRA na UCSAF kwa ukusanyaji mzuri wa mapato.