Habari
Serikali Yaahidi Kuongeza Kasi Kuboresha Mawasiliano kwa Wananchi
Na Mwandishi Wetu, WMTH - Bungeni, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeandaa Mpango unaolenga kutatua changamoto za mawasiliano katika maeneo yote yenye upungufu mkubwa wa huduma hiyo nchini kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini na yale yaliyo nyuma katika mawasiliano ya simu.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhandisi Mhe. Ezra John Chiwelesa, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kutatua Changamoto ya Mawasiliano ya Simu katika Vijiji vya Kata ya Nyamigogo.
Mhe. Dkt. Mkama, amesema Serikali imedhamiria kuondoa changamoto za mawasiliano kwa haraka katika maeneo yote yenye upungufu wa huduma hiyo. Na kuongeza kuwa mpango huo wa dharura unahusisha ujenzi wa minara mipya ya mawasiliano katika maeneo yenye changamoto kubwa za huduma za simu.
Akijibu hoja hiyo, Mhe. Dkt. Mkama alisisitiza kuwa Serikali itahakikisha kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika kupata huduma za mawasiliano, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa kidijitali na kuboresha maisha ya wananchi.
