Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAAHIDI KUIMARISHA USIMAMIZI WA TAASISI ILI KUBORESHA HUDUMA BORA KWA WANANCHI


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dodoma

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itaendelea kuimarisha usimamizi wa taasisi zilizo chini yake ili kuhakikisha zinatoa huduma bora, zenye ufanisi na zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

 

Waziri Kairuki ameyasema hayo tarehe 16 Januari, 2026 wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu ya taasisi nne zinazosimamiwa na wizara hiyo, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.

 

Amesema wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ili kufanikisha utekelezaji wa azma ya uchumi wa kidijitali nchini, sambamba na kuimarisha uwezo wa watumishi kupitia mafunzo ya mara kwa mara, pamoja na kuongeza rasilimali watu pale itakapobainika kuwa kuna uhitaji.

 

Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Selemani Kakoso, ameishauri Serikali kuendelea kuyawezesha mashirika ya umma ikiwemo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Shirika la Posta Tanzania, pamoja na kuyahamasisha kujitangaza zaidi ili kuongeza ushindani na ufanisi katika utoaji wa huduma.

 

Aidha, Mhe. Kakoso ameitaka Serikali kupitia TTCL kupeleka huduma ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia huduma ya Faiba mlangoni kwa Watumishi wa Umma na wananchi ili kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi, hatua itakayochangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa nchi.

 

Vilevile, ameipongeza Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuendelea kupeleka huduma za mawasiliano vijijini, hususan katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara kupitia mradi wa ujenzi wa minara 758, na kuitaka Serikali kuendelea kushughulikia changamoto zilizobaki kupitia utekelezaji wa miradi mingine ya mawasiliano.

 

Kwa upande mwingine, Mhe. Kakoso ameitaka Serikali kuendelea kupanua wigo wa huduma za mkongo wa taifa kwa nchi jirani ambazo bado hazijafikiwa, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na kukamilisha mchakato wa kurusha setilaiti ya taifa unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.